Na Suleiman Abeid, Shinyanga
WAKAZI wa vijiji vinavyozunguka Pori la Akiba Maswa wilayani Meatu Mkoa wa Shinyanga wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti vitendo vya uonevu wanavyotendewa na Askari Wanyamapori katika pori hilo ili kuondoa mivutano ya mara kwa mara.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika Kata ya Sakasaka, diwani wa kata hiyo, Bw.Peter Ndekeja alisema, iwapo Serikali haitachukua hatua za haraka kwa kuwahamisha askari hao kuna uwezekano wa wananchi kujichukulia sheria mkononi ili kukabiliana na vitendo viovu wanavyofanyiwa.
Bw.Ndekeja alisema, kwa kipindi kirefu wakazi wa vijiji vinavyopakana na pori hilo wamekuwa wakisulubiwa kwa vipigo na askari wanyamapori huku wakitozwa fedha kati ya sh. 300,000 na 500,000 bila ya kupewa stakabadhi baada ya kusingiziwa kuingiza mifugo yao ndani ya pori.
Alisema, kati ya wafugaji wanaoishi kando kando ya pori hilo wamepata vilema na wengine kupoteza mifugo yao, baada ya mifugo hiyo kuswagwa na askari hao kupelekwa ndani ya pori ambako ng’ombe hao hupigwa na kuvunjwa miguu, pembe na hatimaye kuliwa na fisi.
Hata hivyo diwani huyo alisema, tatizo linalosababisha mgogoro kati ya wakazi wa vijiji hivyo na askari hao ni kitendo cha kubadilishwa kienyeji kwa mipaka iliyokuwepo awali ambapo hivi sasa alama za mipaka hiyo imesogezwa na kuwekwa ndani ya maeneo ya vijiji.
“Mheshimiwa mgeni rasmi ufumbuzi wa mgogoro huu, kwanza ni kuwahamisha askari wote wanaotuhumiwa kunyanyasa wananchi, lakini pili ni Serikali kupitia upya alama za mipaka ili ieleweke vizuri eneo la Maswa Game Reserve na maeneo ya vijiji, vinginevyo damu hapa itamwagika, wananchi wamechoka kunyanyaswa,” alidai Bw.Ndekeja.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu, Bw. Luhaga Mpina alisema, tatizo la wananchi wa Sakasaka kupigwa na askari wanyamapori limekuwa la muda mrefu hivi sasa na kwamba tayari wamekubaliana na uongozi wa mkoa kufanya utaratibu wa kuwahamisha askari wote wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya unyanyasaji wa wananchi.
Bw.Mpina alisema, amekuwa akisikitishwa na vitendo wanavyotendewa wananchi kwa kisingizio cha kuingiza mifugo yao ndani ya pori hilo la akiba na hata wale wanaokubali kulipa faini huwa hawapewi stakabadhi yoyote ile ya kisheria.
“Ndugu zangu fanyeni subira, tayari malalamiko yenu yanafanyiwa kazi, tumemkabidhi mwakilishi wa mkuu wa mkoa orodha ya askari wote wanaotuhumiwa kuwanyanyasa na kuwapiga wananchi ovyo, tunaamini watafanyia kazi,”
“Sasa tukiona hakuna hatua zinazochukuliwa, Serikali isiwalaumu wananchi watakapoamua kukomesha wenyewe kero hii ya kupigwa, wamekuwa kama watumwa katika nchi yao, hapa tumesema manyanyaso haya yafikie kikomo sasa,” alisema Bw. Mpina.
No comments:
Post a Comment