10 February 2012

Wananchi watambua umuhimu wa kuchunguza afya zao

Na Shekha Seif, Pemba

MKUU wa Kituo cha Ushauri Nasaha Pemba (ZAYADESA), Bi.Fatma Abdalla Faki amesema maudhurio ya wananchi wanaokwenda kuchunguza afya zao kituoni hapo  ni mazuri ukilinganisha na siku za nyuma.

Alisema, jambo ambalo linafanya maudhurio hayo kuwa mazuri ni kutokana na elimu ambayo wananchi wanapata kuhusu umuhimu wa kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.

Hayo aliyasema jana kisiwani Pemba wakati akizungumza na Majira katika mahojiano maalumu ofisini kwake.

Bi.Faki alisema, kituo hicho kimekuwa kikitoa huduma hizo kwa mam wajawazito pamoja na watu wanaotaka kufunga ndoa wakiwemo watu wa kawaida wanaotaka kujua afya zao.

Alisema, suala la mtu kujua afya yake ni jambo la lazima kwani kuna maradhi tofauti ambayo watu wengi yanawapata kama vile kifua kikuu, magonjwa  ya zinaa, homa za mara kwa mara na maradhi mengine.

Alisema, tangu walipokuwa wanafanya ziara za kutembelea sehemu mbalimbali za kutoa elimu watu wengi hivi sasa wametambua umuhimu wa kuchunguza afya zao.

Hata hivyo alisema, suala la utumiaji wa madawa ya kulevya, ulevi wa pombe na bangi nao umechangia maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kwani hupelekea mtu kufanya jambo lolote ambalo anaona kwake ni sahihi hivyo ni vyema kila mwanajamii akaanza kubadilika.

No comments:

Post a Comment