10 February 2012

Mwenyekiti aliyevuliwa gamba aliza wanakijiji

Iringa

WAKAZI wa Kijiji cha Nduli Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mjini mkoani Iringa wameilalamikia hatua ya Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Bw.Lucian Mbosa ya kumfukuza uongozi Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Bw. Ayubu Mwenda bila wao kushirikishwa kwa madai wao ndiyo walimchagua.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo baadhi wanakijiji walidai, wameshangaza na uamuzi wa Katibu huyo kwa kumtimua mwenyekiti wao, ambapo walidai kuwa suala hilo linazingatia masilahi binafsi wakati CCM wana taratibu za kuwafukuza wanachama wake na Serikali inazo taratibu zake za kuwajulisha viongozi na wananchi ambao wanakumbwa na makosa mbalimbali.

"Kama kiongozi wa kijiji, Serikali, chama ama taasisi yoyote ile anaonekana kuwa hafai, unatakiwa kuitishwa mkutano wa hadhara ambao utaridhia makosa na malalamiko yaliyopo kwa mhusika na endapo wajumbe wa mkutano hawatatimia mkutano huo hautakuwa na mamlaka ya kujadili ajenda hiyo, sasa Katibu wa CCM Bw, Mbosa kwa masilahi yake ameamua kumtimua Mwenyekiti wetu bila kutushirikisha makosa yake, hatutakubali kwa hili," alisema Bw, Ibrahim Myovela.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho ambaye alitimuliwa uenyekiti, Bw. Ayubu Mwenda akizungumzia hatua hiyo alisema kuwa hatua ambazo zimechukuliwa dhidi yake ni uonevu kwa sababu Mkurugenzi wa wilaya, Bi.Theresia Mahongo hana taarifa za kutimuliwa na mkutano ambao uliitishwa na CCM chini ya Katibu wa chama hicho, Bw.Lucian Mbosa.

"Tuhuma zote ambazo wananituhumu, hazina ukweli na kama kweli mimi ninazo tuhuma hizo wananchi ni wakweli...wangesema ukweli ilikuwaje, Bw. Mbosa aiitishe mkutano bila kuniarifu na kama ninazo tuhuma ningepewa barua za kuonywa na hatua zingine za kisheria ningechukuliwa, lakini umeitishwa mkutano na kutoa tamko la kunitimua bila kunipa barua, hilo linansikitika," alisema Bw.Ayubu Mwenda.

Mwenyekiti wa CCM tawi la Nduli, Bi. Modesta Mnyenyelwa akizungumzia kutimuliwa kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho alisema, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Iringa Mjini, Bw.Lucian Mbosa aliitisha mkutano katika kijiji hicho ambao ulifanyika jana.

Alisema, awali hawakuarifiwa ajenda za mkutano huo na walishangazwa kuona katibu wa CCM wilaya, Bw. Mbosa akiwaeleza hatua za kumtimua uenyekiti mwenyekiti wa kijiji hicho.

Akizungumzia hatua ya kumtimua uenyekiti, mwenyekiti wa kijiji hicho, Katibu wa CCM wilayani humo, Bw.Lucian Mbosa alikiri kumtimua uenyekiti, Bw.Ayubu Mwenda kutokana na tuhuma ambazo zinamkabili na kuongeza kuwa hatua ambayo ilifikiwa ni halali na iliridhiwa na wanachama wote wa CCM katika kata hiyo kwa madai kuwa alikuwa anakabiliwa na makosa ya msingi.

Katibu huyo alizitaja tuhuma ambazo zinamkabili mwenyekiti wa kijiji cha Nduli Bw.Ayubu Mwenda kuwa ni kutoitisha vikao vya kijiji, kulipwa pesa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Mkoa wa Iringa bila kijiji kujua, kulipwa na kampuni ya simu za mkononi Tigo pesa ambazo huwa anawekewa katika akaunti yake badala ya pesa hizo kuingizwa katika akaunti ya kijiji, kuuza ardhi ya kijiji bila kuwashirikisha wananchi wa Nduli na kusababisha wajumbe tisa CCM kujiuzulu nafasi zao kutokana na kutokuwa na imani na mwenyekiti huyo.

"Tumejaribu kusuluhisha migogoro hiyo hapo kijijini bila mafanikio na wananchi wamepiga kura ya kumkataa mwenyekiti wao ambapo kura nyingi za wakazi wa Nduli zilionesha kutokuwa na imani na Bw, Ayubu na kumtaka aachie ngazi ya uenyekiti kwa hiyo mimi niliidhinisha maamuzi ambayo yalitolewa na wananchi ambao pia ni wanachama wakazi wa Nduli," alidai Katibu huyo.
**************
ANCHOR
Mpango wa CCM
wabadilika

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikianza rasmi mchakato wa uchaguzi wa viongozi wake kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa, chama hicho kimetangaza utaratibu mpya wa maombi ya nafasi kwa ngazi ya shina ambapo sasa mabalozi hawatajaza tena fomu.

Akitangaza utaratibu mpya wa zoezi zima la uchukuaji fomu za maombi ya kutaka kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Kapteni Mstaafu, John Chiligati mkoani Shinyanga alisema, katika uchaguzi wa mwaka huu wagombea wa ngazi ya shina hivi sasa wataandika barua za maombi.

Bw.Chiligati ambaye alikuwa akizungumza katika maadhimisho ya sherehe za CCM kutimiza miaka 35 zilizofanyika hivi karibuni kimkoa katika Kata ya Mwawaza Manispaa ya Shinyanga alisema, hivi sasa wana CCM wanaotaka kugombea uongozi katika ngazi ya shina hawatatakiwa tena kujaza fomu kama ilivyo kuwa zamani.

Alisema, wagombea wa ngazi ya shina na matawi hawatatozwa fedha zozote kwa ajili ya kuchangia gharama za uchaguzi na badala yake kwa wale wa mashina wataandika barua zao na kuzikabidhi kwa Katibu wa tawi katika eneo husika bila kutozwa fedha zozote na ngazi ya tawi.

Hata hivyo alisema, ngazi ya tawi Wanaccm wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za tawi wao watapaswa kujaza fomu na kuziwazilisha kwa katibu kata wa eneo husika ambapo aliwatahadharisha wana CCM wote kutokubali kutozwa fedha zozote katika ngazi hizo mbili.

“Ndugu zangu CCM katika uchaguzi wa mwaka huu tuna mabadiliko kidogo, na mabadiliko haya yanahusu ngazi ya mashina na matawi, kwa ngazi ya shina yeyote anayetaka kugombea hatakiwi kujaza fomu, ataandika tu barua na kuelezea nia yake ya kutaka kuwa kiongozi na kumkabidhi katibu wa tawi lake, hakuna mchango,”

“Vile vile kwa ngazi ya Tawi, japokuwa wagombea katika eneo hili watajaza fomu, lakini pia hakuna suala kuchangia gharama za uchaguzi, fomu ni bure, yeyote atakayewatoza fedha huyo ni mwizi, hatutaki fedha iwe kizuizi cha kumzuia mwana CCM kugombea uongozi,” alifafanua

Bw.Chiligati alisema ,uchangiaji wa gharama za uchaguzi utaanza kwa ngazi ya kata, ambapo kila mwana CCM anayetaka kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa kata, atapaswa kuchangia kiasi cha sh. 10,000 ili aweze kupewa fomu za kugombea.

Vivyo hivyo kwa ngazi za wilaya, mkoa hadi Taifa kutakuwa na uchangiaji wa gharama za uchaguzi kwa kadri gharama zake zitakavyopangwa ambapo pia suala wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) sasa watachaguliwa kutoka kila wilaya badala ya utaratibu wa zamani ambapo kila mkoa ulitoa mjumbe mmoja.

Kwa upande mwingine, Bw. Chiligati aliwataka wana CCM kuhakikisha wanawachagua viongozi waadilifu ambao ni wachapa kazi na kuachana na wale wote ambao wamekuwa wakikipaka chama matope kutokana na vitendo vyao viovu.

No comments:

Post a Comment