07 February 2012

Wakazi Mabwepande waandamana hadi Ikulu


Wakwama kumuona JK
Na Salim Nyomolelo
ZAIDI ya wakazi 100 waliovunjiwa nyumba zao Kijiji cha Mabwepande, kilichopo Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, kupisha waathirika wa mafuriko, jana waliandamana hadi Ikulu ili kufikisha kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete.

Wakizungumza na Majira jirani na ukuta wa Ikulu, waathirika hao walisema walifikia uamuzi huo baada ya kuvamiwa na polisi saa sita usiku wa kuamkia jana na kuambiwa waondoke eneo hilo.

Miongoni mwa wakazi hao Bw. Mohammed Madebe, alisema polisi hao walivamia katika maeneo waliyojisitili, kuwaondoa kinguvu na kuwapiga wakati wakisubiri majibu ya madai yao.

“Kimsingi tumechoshwa kunyanyaswa hivyo tumeamua kuja Ikulu kuonana na Rais Kikwete kwa sababu watendaji wake wanatabia ya kupotosha ukweli baada ya kusema sisi tunahitaji fidia jambo ambalo si kweli, tunachotaka ni kupatiwa makazi ya kuishi si vinginevyo,” alisema Bw.Madebe.

Naye Bi.Dumitima Kagoma, alisema wamekuwa wakiishi chini ya miti tangu Januari 11 mwaka huu, baada ya nyumba zao kuvunjwa na kufungwa mahema kwa ajili ya waathirika wa mafuriko.


Wakiwa katika eneo la Ikulu, wakazi hao waliteua wawakilishi watano ili waweze kuonana na rais ili kuwasilisha madai yao.

“Tulipofika hapa getini, tulifanikiwa kuonana na mtu ambaye alijitambulisha kuwa ni Ofisa Usalama bila kutaja jina lake na sisi hatukusita kumweleza kilio chetu,” alisema Bi.Skondia Joseph.

Alisema ofisa huyo aliwataka wawakilishi wao waingie ndani na wengine wakasubiri katika bustani iliyopo Posta ya zamani.

Bi.Joseph alisema baada ya wawakilishi wao kurudi, waliwaeleza kuwa juhudi za kuonana na Rais Kikwete zimeshindikana ambapo majibu waliyopewa na Ofisa Usalama ni kwamba, suala lao linafahamika kuanzia ngazi ya mtaa hadi kwa rais, hivyo linashughulikiwa kwa umakini zaidi.


1 comment:

  1. Wananchi wa mabwepande... nawasihi muone imani kwa kiongozi wenu, mizigo mingi anayo hawezi tena kuibeba kama alivyoahidi wakati Ari na Nguvu zilikuwa mpya mpya, "Amechoka jamani" mwacheni.
    Si vizuri kumwona kiongozi mheshimiwa akilia kwa kuzidiwa na matatizo.

    ReplyDelete