07 February 2012

Mbatia akubali yaishe, afuta kesi dhidi ya Mdee


Na Peter Mwenda

CHAMA cha NCCR-Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), vimekubaliana kufutwa kwa kesi ya kupinga matokeo ya ubunge katika Jimbo la Kawe, Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, dhidi ya mbunge wa sasa kwa tiketi ya CHADEMA, Bi.Halima Mdee.

Muafaka huo ulitangazwa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt.Willibrod Slaa na Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Bw.Samwel Ruhuza.

Wakizungumza na waandishi wa habari, viongozi hao walisema kesi hiyo namba 100/2010 imefutwa rasmi jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo walalamikaji na walalamikiwa, waliweka saini zao na kila upande utabeba gharama zake.

Dkt.Slaa alisema, CHADEMA imefurahishwa na uamuzi wa chama hicho kukubali kufuta kesi hiyo bila kutaka gharama yoyote waliyoitumia kufungua shauri hilo.

“Uamuzi huu umetokana na mapenzi ya vyama hivi kujali maslahi ya Watanzania zaidi kuliko ya chama, makubaliano ya kufuta kesi hii ni historia kubwa na ya kwanza kufanyika nchini,” alisema.

Aliongeza kuwa, lengo la vyama vya upinzani ni kuiondoa CCM madarakani hivyo makubaliano hayo ni ushindi dhidi ya ubinafsi ambao wapinzani wakiruhusu makundi, hakutakuwa na mafanikio ya kuleta mabadiliko nchini.

Alisema Bi.Mdee hakuwepo katika muafaka huo kwa sababu yupo bungeni lakini amewakilishwa na mawakili wake.

Akijibu hoja kwanini wasiwasamehe madiwani waliowafukuza mjini Arusha, Dkt.Slaa alisema, kesi ya madiwani hao inatokana na kosa la kinidhamu ambapo CHADEMA haiwezi kuruhusu uvunjwaji  katiba ambayo wamekubaliana kuifuata.

“Hoja iliyopo bungeni kwa sasa ni kupata Katiba Mpya, naomba Watanzania wajiandae kutoa maoni yao bila woga, hoja ya wabunge kuongezwa posho kwa kazi ya kukaa bungeni hailingani na kazi ya madaktari waliogoma wakidai posho zaidi,” alisema.

Bw. Mbatia katika kesi hiyo, alikuwa akiwakilishwa na wakili Bw.Mohammed Tibanyendera, kutoka Kampuni ya Star Chambers Advocates ambapo Bi.Mdee, alikuwa akiwakilishwa na wakili  Bw.Mabere Marando na Bw.Edson Mbogoro ambao wote walikuwepo katika mkutano huo.

1 comment:

  1. Big up Mheshimiwa Mbatia. Hiyo ni ishara nzuri ya kukomaa kisiasa. Pia inaonyesha kama alivyosema mheshimiwa Slaa, upendo na umoja. Kukiwa na Upend ,Umoja na mshikamano Shetwani liitwalo CCM kamwe halitoweza kuendelea kuisambaratisha nchi yetu Takatufu.'Rasilimali ya Mnyonge ni umoja'.
    Together we stand devided we fall.
    Mungu Ibariki Tanzania.

    ReplyDelete