07 February 2012

Chiligati: TAKUKURU kamateni wala rushwa ndani ya CCM

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewaagiza Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kuwakamata wana CCM wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Tanzania Bara, Kapteni mstaafu Bw.John Chiligati, alitoa agizo hilo juzi katika maadhimisho ya sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa kwa chama hicho ambazo kimkoa zilifanyika katika Kata ya Mwawaza, Manispaa ya Shinyanga.

Alisema vitendo vya rushwa vinachangia kukichafua chama hicho na kusababisha Watanzania wakichukie kwa madai ya kuongozwa na mafisadi hivyo aliwataka wanaCCM, kutumia mwanya wa uchaguzi ndani ya chama hicho kuwachuja wale wagombea wanaotaka uongozi kwa kununua kura.

“Kuanzia sasa, chama chetu kinawaagiza Maofisa wa TAKUKURU nchini kuanza kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wana CCM wote bila kujali nyadhifa zao ambao wameanza kuwashawishi wapiga kura kwa kuwapa fedha ili wachaguliwe katika uchaguzi unaotarajiwa kuanza mwezi huu.

“Ndugu zangu, suala la rushwa limekuwa likipigiwa kelele na chama chetu lakini wapo baadhi ya watu ambao wameshindwa kujiepusha na vitendo hivi ambavyo vinatukera sana, suala hili ni aibu kubwa ndani ya chama chetu na limetuchafua sana,” alisema.

Alisema dhamira ya chama hicho ni kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa kuanzia ngazi ya mashina, wanakuwa safi na waadilifu wasio na harufu ya rushwa.

“TAKUKURU kamateni mtu yeyote bila kumwogopa kama itabainika anatafuta uongozi kwa kutoa fedha (rushwa), wana CCM tusaidiane katika hili, ukimuona mtu anatoa rushwa au anataka kununua kura mtaje bila kuogopa ili akamatwe na kufikishwa mahakamani,” alisema.

Bw.Chiligati alizionya kamati na viongozi wote wa CCM ambao watasimamia uchaguzi huo, kuhakikisha wanatenda haki bila kuwabagua wanachama kwa misingi ya fedha.

Aliwaonya wanachama wenye tabia ya kuomba fedha kutoka kwa wagombea kwani kama watabainika, nao watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Tumeamua kupambana na kero ya rushwa, yule ambaye anaona hawezi vita hii, tunamuomba atoke ndani ya CCM, atafute chama kingine, tutumie uchaguzi huu kusafishana ili tupate viongozi wazuri na wachapa kazi, wabaya wote waachwe pembeni,” alisema.

Akizungumzia mabadiliko ya katiba nchini, Bw.Chiligati aliwataka wakazi wote wa Shinyanga, kushiriki kikamilifu kutoa maoni yao juu ya Katiba Mpya kwa uhuru bila ya kumuogopa mtu.

Alisema mara baada ya Rais Jakaya Kikwete kuteua tume ya kukusanya maoni, kila mwananchi atajitokeza kutoa maoni yake bila kuzuiwa na mtu ili kueleza anataka katiba mpya ijayo iweje.

4 comments:

  1. MBONA CCM KARIBU WOTE NI WALA RUSHWA, BASI WOTE MTAKAMATWA!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. MBONA CCM KARIBU WOTE NI WALA RUSHWA, BASI WOTE MTAKAMATWA!!!!
    Hii Inamaana kuwa chama kitakosa viongozi, wote watakuwa jela...

    ReplyDelete
  3. Chiligati ni nani aamuru TAKUKURU kukamata wararushwa wa CCM,yeye ndiye amewajiri au TAKUKURU ni mali ya CCM?.Kauli yake ni udhalilisahji wa chombo cha umma na Serikali.CCM ni chama tu kama chama cha kufa na kuzikana na uanachama wake ni wa hiari.Kama kuna wanachama wanakula rushwa ni jukumu lao kuwakamata na wakuwashughulikia. Hata hivyo viongozi wengi wa CCM ni walarushwa ,hivyo watakamata wote kuanzia mwenyekiti taifa na mjumbe wa shina.

    ReplyDelete
  4. Hawa ndiyo Watawala wetu ( Chiligati ). Mara anamtangaza mwenzao katika CHAMA eti siyo raia wa Tanzania. Sasa huyu huyu anataka TAKURURU ifanye kazi yake. Sijui siku zote ilikuwa inafanya kazi gani.
    Tuna matatizo makubwa hapa nchini, kama hawa ndiyo watawala wetu.

    ReplyDelete