Na Mwajabu Kigaza, Kigoma Vijijini
SHIRIKA lisilo la kiserikali KIOO lililopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji limetumia kiasi cha milioni 93.2 kwa lengo la kuwapatia elimu viongozi wa Serikali juu ya madhara ya rushwa, utekelezaji ambao umeanzia Wilaya ya Kigoma Vijijini.
Mratibu wa mradi huo, Bw.Saimoni Edward amesema warsha hiyo iliwashirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo maofisa wa polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), idara za Serikali na watendaji wa kata.
Bw.Edward alisema, mradi huo ulifadhiliwa na Ubalozi wa Finland nchini ili kutoa elimu hiyo kwa viongozi na jamii ambapo itasaidia kupunguza tatizo la rushwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema, kupitia mradi huo mkakati thabiti utaanzishwa kwa kuunda vikundi vya wapinga rushwa katika kila kata za mradi ili kuelimisha jamii juu ya rushwa na hatua zipi za kuchukua.
Bw.Edward alitaja baadhi ya kata mbazo mradi huu utatekelezwa ikiwa ni pamoja na Kagunga, Mwamgongo, Kagongo, Bitale, Mwandiga, Mahembe, Ilagala na Sunuka ambapo vijiji vyote vipo katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma Vijijini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Bw. Hamisi Betese ambaye alikuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo aliwataka viongozi hao kutumia vyema mafunzo hayo katika kuelimisha jamii ambayo haijafanikiwa kujua elimu hiyo na sio kuishia kupokea posho tu.
No comments:
Post a Comment