15 February 2012

Wanafunzi 330 wanakaa chini Rutale-Utafiti

ZAIDI ya wanafunzi 330 katika Shule ya Msingi Rutale Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma wanakalia sakafu wakati wa masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukumbwa na tatizo la ukosefu wa madarasa ya kutosha, matundu ya vyoo na madawati.

Uchunguzi uliofanywa na Majira baada ya kufika shuleni hapo hivi karibuni uligundua kuwa darasa moja huwa linakusanya wanafunzi wa mikondo mitatu, sawa na wastani wa wanafunzi 135 kwa darasa, badala ya 40.

Mbali na hayo uchunguzi huo ulibainisha kuwa jumla ya wanafunzi 952 shuleni hapo wanategemea matundu nane pekee ya choo, jambo ambalo wanafunzi hao walidai kuwa huwa linawanyima fursa ya kutumia vyoo kama inavyostahili, hivyo kuteseka.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambayo ilitokana na mgawanyiko wa Shule ya Msingi Ujiji mwaka 2007, Bw.Abed Mabyana alisema, matatizo hayo yanasababisha msongamano mkubwa na hata hali ya ufundishaji kuwa ngumu kutokana na msongamano wa wanafunzi hao.

Baadhi ya wanafunzi ambao walizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti shuleni hapo waliiomba Serikali wakiwemo wahisani mbalimbali kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika shule hiyo huduma mbalimbali wanazohitaji ili waweze kuyafikia malengo yao hususani ujenzi wa vyoo, vyumba vya madarasa, yakiwemo madawati.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Bw. Protas Kato alikiri kuwepo tatizo hilo shuleni hapo, huku akisisitiza kuwa, ufinyu wa bajeti ndiyo kikwazo katika kufanikisha malengo, lakini muda si mrefu tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi.

"Hayo matatizo tutayatatua kikamilifu kwa mwaka huu wa fedha, ambapo halmashauri yetu itakuwa imetengewa kiasi cha fedha katika bajeti, ili kiweze kutumika kutekeleza mpango huo," alisema.

Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Shule za Msingi Manispaa ya Kigoma Ujiji, Bw. Aroan
Kagulumjul alisema, katika manispaa hiyo shule nyingi zinakabiliwa na upungufu wa jumla ya madawati 654, matundu ya vyoo 1,553, madarasa 668 na nyumba za walimu 1,006.

No comments:

Post a Comment