Na Mwandishi Wetu, Kigoma
MKUU wa Wilaya ya Kigoma, Bw.John Mongella amekitaka Chama cha Wakulima wa Mchikichi Mkoa wa Kigoma (KIPAFADA) kutekeleza malengo iliyojiwekea katika kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo unawanufaisha wakulima wake kutokana na hali duni waliyonayo wakulima wa zao hilo.
Mwito huo aliutoa hivi karibuni wakati akizindua mradi wa uhamasishaji na ushirikishaji jamii katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofadhiliwa na Shirika la Foundation For Civil Society mkoani humo kwa gharama ya sh.milioni 45.
Alisema, bado zao hilo halijaleta tija kwa wakulima kutokana na wakulima wengi kutotaka kubadilika katika matumizi ya mbegu bora na zana za kisasa wakati wa kusindikia mazao ya michikichi kutokana na hofu ya kukimbia gharama na hivyo kuzidi kubaki kuwa maskini.
Akitoa mfano wa mafanikio ya zao hilo alisema, nchi ya Malaysia ilitoa mbegu ya zao hilo kutoka mkoani Kigoma na kwa sasa ndiyo mzalishaji na msambazaji mkubwa wa mazao yanayotokana na zao la michikichi yakiwemo mafuta ya mawese ambayo Tanzania imekuwa ikiagiza kiasi kikubwa cha mafuta hayo kutoka nchini humo.
"Ili kukabilina na hali hiyo Serikali kwa kutumia wataalamu wake katika ngazi mbalimbali ikiwemo halmashauri, Serikali ipo tayari kushirikiana na chama hicho katika kuhakikisha kuwa zao la michikichi linakuwa moja ya mazao makuu katika kuwaondolea umaskini wananchi wa mkoa huu," alisema
Akizungumza katika uzinduzi huo Mwenyekiti KIPAFADA, Bw. Elias Kituye alisema, licha ya Mkoa wa Kigoma kuwa moja ya mikoa inayolima kwa wingi zao la michikichi linalotumika kuzalishia mafuta ya mawese bado wakulima wengi hawajanufaika vya kutosha na zao hilo.
Alisema, muda mwingi mashamba makubwa ya zao hilo yameendelea kuwa na miche ile ya zamani ambayo huzalishaji wake ni kidogo na kwamba kwa sehemu kubwa kwa sasa zao hilo linalimwa kama sehemu ya kujitafutia fedha za kujikimu kimaisha na siyo kuyafikia malengo mengine yanayojikita kwa upande wa maendeleo.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa tatizo lingine ambalo bado linawakabili wakulima wa zao hilo mkoani humo ni utumiaji wa zana duni za kusindikia ambazo huzalisha mafuta yasiyokidhi viwango na hivyo kusababisha kutokuwa na soko la uhakika.
Alisema, chama chake pamoja na mipango mingine kimeanza mkakati wa uhamasishaji wa matumizi ya mbegu bora aina ya Tenera kwa kutumia zana za kisasa za kuzalishia mawese ambapo mpango huo unafanywa kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogovidogo nchini (SIDO).
No comments:
Post a Comment