02 February 2012

Utafiti uende sanjari na utatuzi wa matatizo yanayowasibu watoto

Na Rachel Balama

TAFITI mbalimbali zimekuwa zikifanyika kuhusiana na mambo mbalimbali kwa lengo la kupata ufumbuzi wa mambo hayo.


Kama tunavyojua tafiti huwa zinagharimu fedha nyingi sana na wananchi wengi wanategemea kwamba mara tafiti zinapokamilika na ripoti kutolewa wanatarajiwa kupatiwa ufumbuzi wa mambo ambayo yalikuwa yanafanyiwa utafiti.

Kwa mtazamo wangu japo tafiti zimekuwa zikifanywa na ripoti kutolewa lakini bado utekelezaji wa ufumbuzi wa matatizo una kuwa ni mdogo.

Hivi karibuni Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kukuza, kuendeleza haki na maendeleo kwa watoto, vijana na wanawake linafanya tafiti wa miji salama kwa watoto Tanzania.

Utafiti huo unafanyika kwa ushirikiano na Shirika la Kulinda na Kutetea Watoto la Kimataifa-UNICEF,Wizara ya Maendeleo, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Taasisi zisizo za kiserikali kwa pamoja na watoto.

Katika utafiti huo unatarajia ifikapo mwakani itatolewa ripoti sambamba na ripoti ya dunia kuhusu utafiti wa miji salama kwa watoto.

Utafiti wa Tanzania utaangalia kwa upana jinsi miji inavyokuwa na kupanuka na namna inavyoathiri asili ya makazi na ukazi wa familia zilizoko mijini na vijijini.

Pia itaangalia tofauti za kimaisha zilizopo kati ya miji na vijiji na utofauti wa kipato kati ya makundi ya kijamii waishio mijini na vijijini.

Mkazo utaangalia kwenye masuala ya msingi ya haki za mtoto ikiwemo suala la afya, lishe, ulinzi wa mtoto, elimu, usafi wa mazingira, maambukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI, makazi na uwakilishi wa watoto.

Ripoti hiyo pia itaeleza kinagaubagafaida zilizopo za maisha ya mijini ikiwemo lile la kuongezeka kwa fursa za huduma za kijamii pamoja na kudadavua matatizo na changamoto wanazopata watoto wanaokuwa mijini huku wakipambana na msongamano na mazingira machafu.

Umasikini uliokithiri, kazi hatarishi na ngumu, utumiaji wa madawa, uvunjaji wa sheria na utendaji wa makosa, makundi mabaya,unyonywaji kijinsia, uteswaji, ukatili, unyanyaswaji na usafirishwaji.

Maeneo mengine yatakayoangaliwa na ripoti ni lile la watoto waishio kwenye mazingira  hatarishi, watoto wanaoishi kwenye nyumba zenye maisha ya chini, watoto wasiojiweza(wenye ulemavu), watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani, watoto wanaotumikishwa majumbani.

Pia itaangalia namna ambavyo athari za kiuchumi na matatizo ya kimazingira jinsi yalivyoathiri watoto na familia zao yakiwemo matatizo ya umeme, uchafuzi wa hali ya hewa, maji na upandaji wa gharama za vyakula, umeme, usafiri na huduma za kiafya na kibinadamu.

Ni kwa kiwango gani watoto wanapata fursa ya kuwa  na viwanja vya michezo, uwezo wa kushiriki michezo na burudani na fursa zamawasiliano na kuangalia kwa namna gani wataalamu wa mipango miji na watoa maamuzi wanazingatia kwa upana maswala ya watoto katika mazingira ya mijini.

Mpango kazi wa utafiti huo ni kutafutataarifa zilizopo hapa Tanzania zinazohusiana na miji, kushirikiana na washirika wa mradi katika upangaji wa hatua za awali za mpango wa utafiti.

Kupanga muda, maeneo, kuanda madodoso na kuwauliza walengwa mbalimbali wakiwemo wanajamii, vikundi vya watoto, watoto walio nje  na mashule, warsha zitakazo husisha watoto, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, kidini, kijamii, kiserikali, wafanyakazi wa serikali wanaofanya kazi kwenye idara za kupambana na umasikini, afya, elimu, ulinzi  wa watoto.

 UKIWMI na wale wanaofanyakazi katika masuala ya watoto katika miji, vikundi vya vijana na wale wa kampuni binafsi na viongozi.

Kimsingi ripoti hiyo itakuwa na mambo mengi kutokana na taarifa mbalimbali kuhusiana na suala la miji na usalama wa watoto.

Taarifa zingine zitakazopatikana na maswali watakayoulizwa watu mbalimbali, vikundi vya mijadala, warsha za ukusanyaji maoni, majadiliano kwa makundi.

Maeneo ya utafiti ni mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.

Ni jambo jema kwa Shirika hilo kutafiti matatizo yanayowasibu watoto lakini ni vizuri pia baada ya utafiti tuone kwa vitendo watoto hao wakisaidiwa na kuondokana na matatizo.

No comments:

Post a Comment