Rachel Balama
KUMEKUWEPO na migogoro mingi kati ya wananchi na wawekezaji ambayo inatokana na wananchi kutonufaika na rasililimali za migodi zinazowazunguka.
Hali ya wananchi kutonufaika na rasilimali za migodi zilizopo kwenye maeneo yanayowazunguka ni chanzo kikubwa cha kuzuka kwa migogoro katika maeneo hayo.
Hata hivyo migogoro inapozuka serikali imekuwa ikikaa kimya pasipo kutafuta ufumbuzi jambo linalopelekea wananchi kuwa na visasi na wawekezaji wanaofika nchini.
Utakumbuka Mei, mwaka huu lilitokea tukio katika mgodi wa North Mara ambapo watu watano waliuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi ambao walivamia mgodi huo kwa lengo la kuiba mchanga wa dhahabu .
Mbali na hilo la Mei, mwaka huu hata mwaka 2009 liliwahi kutokea tukio la polisi kuwaua watu ambao walidaiwa kuingia kwenye mgodi huo kwa lengo la kuiba mchanga.
Lakini ukweli utabaki kwamba vitendo vya watu kuvamia mgodi na kuingia kwa lengo la kuiba mchanga vinasababishwa na serikali kutoweka mazingira mazuri kwa wananchi wanauzunguka mgodi huo kunufaika na rasilimali zilizopo.
Polisi wamekuwa wakiripotiwa kuua raia kutokana na sababu mbalimbali lakini kubwa likiwa ni majambazi.
Wanaharakati na watu mbalimbali wamekuwa wakipiga kelele kwa lengo la kukemea mauaji yanayofanywa na watu dhidi ya watu wengine, polisi dhidi ya raia kwa kuwa ni kitendo cha kujichukulia sheria mkononi.
Baadhi ya polisi wamekuwa wakikiuka haki za binadamu kwa kufanya vitendo vya ukatili na kisha uongozi wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi umekuwa ukiwakingia kifua polisi hao kwa kudhurumu haki za raia kuishi.
Mbali na mauaji ya Tarime, ni mara ngapi tumeshuhudia polisi wanapomkamata raia na raia huyo kuonekana hana hatia polisi husingizia eti wamemkamata na kete kadhaa za misokoto ya bhangi.
Polisi utoa visingizio hivyo ili mradi tu kukwepa fedheha kwa jamii pale wanapoonekana kwamba wamefanya kosa bila sababu za msingi.
Japo watu waliouwawa walikuwa ni waharifu kwa kuvamia mgodi kwa lengo la kuiba lakini polisi walitakiwa kutumia mbinu mbalimbali walizofundishwa juu ya kukabiliana na majambazi na sio kuua kama walivyofanya.
Japo watu hao nao walikuwa wakitumia siraha za jadi lakini polisi walipaswa kutumia mbinu kwa lengo la kukabiliana nao.
Lakini kama hali itaendelea kuwa hivyo basi kwa Tarime watu wataendelea kupoteza maisha kila kukicha kwa kuwa wataendelea kuvamia mgodi na kutaka kuiba na polisi nao watawaua pale watakapoonekana kufanya hivyo.
Watu hao walivamia mgodi huo kwa lengo la kuiba kutokana na serikali kutowatengenezea mazingira mazuri ya wananchi wa Tarime kunufaika na rasilimali zilizopo.
Katika kukabiliana na matatizo hayo serikali ni vyema ikawa makini katika kutatua tatizo kuliko kulikumbatia tatizo kwani linaweza kuwa kubwa na kushindwa jinsi gani ya kukabiliana nalo.
Ukweli ni kwamba kinachotakiwa kufanyika Tarime viongozi kutolichukulia tatizo hilo kuwa la kisiasa ili watu wasiendelee kuuwawa kila kukicha.
Japo siasa imeingilia kati suala hilo ila serikali iwe na mtizamo chanya kujenga uchumi wa nchi ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali zao.
Serikali inapaswa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya migodi wananufaika na rasilimali hizo ili kuepusha migogoro inayojitokeza.
Kutokana na wananchi walio wengi kutofaidika na rasilimali ambazo zipo kwenye maeneo yao ndio maana tumejikuta tukiingia kwenye migogoro inayopelekea watu kuuana.
Ni kikwazo kikubwa sana kinachokatisha tamaa ya kuwepo wa rasilimali harafu wananchi hawanufaiki nacho.
Serikali iangalie uwezekano wa mtanzania kupewa fursa ya kumiliki kitu chenye manufaa zaidi tofauti na sasa ambapo mtanzania hawezi kupewa fursa hiyo.
Tumekuwa tukishuhudia kila kukicha migogoro ya ardhi inayoendelea nchini na hiyo inatokana na wananchi kutopewa fursa ya kumiliki vitu hivyo.
Ili kuondoa matatizo hayo kwa wananchi kuuana kwa ajili ya kugombea rasilimali huenda kwa kupigana wenyewe kwa wenyewe au kupigwa na polisi kunakosababishwa na matatizo ya rasilimali iko haja ya serikali kutenga eneo la wachimbaji wadogo ambao hawataingiliwa na wawekezaji wakubwa.
Kwa kufanya hivyo migogoro inayoendelea kila kukicha sehemu za migodini itapungua kama si kwisha.
Pia jinsi ya uwajibikaji wa jeshi la polisi wakati mwingine polisi wamekuwa wakiukaji wa haki za binadamu kwa kuwapiga watu pasipo na sababu za msingi.
Ni vyema Jeshi la polisi liwajibike ipasavyo pasipo kuvunja haki za binadamu ili hali ya ubinadamu iwepo na haki itendeke.
Ukiukwaji wa vitendo vya haki za binadamu katika mgodi wa Nyamongo vinafanyika kwa hali ya juu na vinachangia kuleta machafuko baina ya watu na wawekezaji, wananchi na polisi.
Ni vyema yaliyotokea katika Mgodi wa North Mara, yasipuuzwe na badala yake yafanyiwe uchunguzi wa kina ili kujua nini tatizo ili kutafuta njia mbadala itakayowanusuru raia wasindele kufa na kuacha vitendo vya kuingia mgodini kwa lengo la kuiba mchanga.
Endapo utafiti wa kina utafanyika na kugundua nini tatizo linalopelekea watu kuvamia migodi kwa lengo la kuiba linaweza kutafutiwa ufumbuzi ili matatizoyasiendelee.
Mwisho
No comments:
Post a Comment