02 February 2012

MAAFISA KUHAMISHWA VITUO VYA KUFANYIA KAZI

Na Salim Nyomolelo

WIZARA ya Mambo ya Ndani imesema kuwa maafisa uhamiaji wasiotimiza wajibu wao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kuwahamisha vituo vyao vya kazi.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa wizara hiyo Bw.Shamsi Vuai Nahodha baada ya kuzindua kamati ya Taifa ya kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu.

Bw.Nahodha alisema alitoa muda wa mwezi mmoja kuhakikisha kuwa maafisa wa uhamiaji wanajirekebisha kutokana na kashfa ya kuingiza wahamiaji haramu kinyume cha taratibu.

Alisema licha ya kuwa muda huo bado kukamilika lakini tayari alipata ripoti ambazo zinaeleza namna watakavyo boresha utendaji kazi huo.

Alisema baada ya kutoa muda huo kitengo cha uhamiaji jijini Dar es salaam kimeweza kuongeza mapato ikilinganishwa na vya mkoani.

Alisema hakulizika na mapato yaliyokusanywa katika mikoa ya Arusha,Kilimanjaro,Mbeya,Mara na Kagera kwa sababu ndio inapakana na nchi za jirani ikilinganishwa na Dar es Salaam.

"Nimemuagiza katibu mkuu aangalie taratibu za utumishi ili kuwahamisha maafisa uhamiaji katika mikoa hiyo wenye uwezo mdogo kiutendaji",alisema

Akizungumzia suala la kamati hiyo Bw.Nahodha alisema ameunda kamati ya wajumbe 19 ambayo inaongozwa na mwenyekiti Bw.Kinemo Kihonamo ili kuthibiti usafirishaji haramu wa binadamu iliundwa kwa kifungu cha sheria namba 30 na 31 ya mwaka 2008.

Alisema usafirishaji haramu wa binadamu una uhusiano mkubwa na madawa ya kulevya pamoja na uingizwaji wa silaha nchini.

Alisema baada ya kuundwa kwa kamati hiyo wataanza kufanya msako kwa wahamiaji hao kwa kutumia helkopta.

"Kuna idadi ya wahamiaji haramu wapatao 3000 ambao wanaharibu bajeti ya serikali katika kuwahudumia chakula,maradhi na matibabu",alisema

Aidha waziri alisema tafiti za kina zinaonyesha kuwa usafirishaji haramu huo unawaingizia fedha nyingi ambapo jumla ya dola za kimarekani 32 kwa kila mwaka.   

mwisho.

No comments:

Post a Comment