15 February 2012

TFF yamshauri Wambura kuweka pingamizi DRFA

Na Zahoro Mlanzi

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imemshauri aliyekuwa Katibu Mkuu wa FAT (sasa TFF), Michael Wambura kama anaona kuna mgombea hana sifa za kuwania uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salam (DRFA), ni vizuri akaweka pingamizi kwa kamati husika.

Hatua hiyo imetokana na Wambura, kupeleleka malalamiko yake kwa TFF juu ya mchakato wa uchaguzi wa chama hicho unaoendelea hivi sasa, kwamba una upungufu kutokana na baadhi ya vipengele vya katiba ya DRFA havifanani na ile ya TFF.

Kwa mujibu wa Wambura, ambaye alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari alidai kuna kipengele katika katiba ya DRFA kinachoelezea kwamba kuna elimu nyingine inayofanana na kidato cha nne, kitu ambacho ndicho anachopinga.

Akilitolea ufafanuzi suala hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura alisema kamati ilikutana juzi na kuamua kumshauri Wambura kama anaona kuna mgombea hana sifa katika uchaguzi huo ni bora aweke pingamizi kwa kamati husika.

"Kamati imemshauri Wambura ni bora afuate taratibu zinazotakiwa kwa kuanzia chini na kisha kuja juu, hivyo katika suala hilo ameshauriwa kama anaona kuna mgombea hana sifa ni bora aweke pingamizi kwa Kamati ya Uchaguzi ya mkoa husika," alisema Wambura.

Wakati huohuo, Wambura alisema timu ya Manyoni FC ya Singida, imeshindwa kutokea kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Polisi Tabora, iliyokuwa ichezwe Jumapili kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, hivyo imeshushwa daraja.

Alisema kwa mujibu wa kanuni ya 21 ya FDL, timu yoyote inayoshindwa kufika kituoni na kusababisha mchezo husika kutochezwa itashushwa daraja hadi Ligi ya Taifa na matokeo ya michezo yake yote itafutwa, ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye mashindano.


No comments:

Post a Comment