Na Mwali Ibrahim
MKURUGENZI wa bendi ya Extra Bongo 'Next level', Ally Choki amesema haoni umuhimu wa tuzo za Muziki za Kilimanjaro (Kili Music Awards) kwa kuwa zipo kwa ajili ya watu maalumu.
Licha ya kukerwa na tuzo hizo, Choki ameingiza nyimbo mbili katika tuzo za mwaka huu, kwenye kipengele cha Wimbo Bora wa Kiswahili wa bendi, ambazo ni Mtenda hakitendewa na Falsafa ya mapenzi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Choki alisema hana mpango na tuzo hizo hata kama nyimbo zake, zikichukua tuzo kwani haoni uthamani wake kwa kuwa waandaaji hawatendi haki katika kuchagua.
"Sina mpango hata na tuzo zenyewe na hata kama wimbo wangu utachukua, mimi sitajali kwani tuzo hizi zipo kwa ajili ya watu fulani na wengine wamewekwa tu, ili kuwasindikiza wengine hivyo sina imani nazo kwani nina uhakika na nanichaokisema kuwa zipo kwa ajili ya watu fulani," alisema.
Akitolea mfano wa tuzo zilizopita, ambapo yeye aliingiza wimbo wa Mjini mipango ukiwa katika kipingele hicho, lakini alishangaa kusikia maneno kuwa amejitoa bila hata yeye kujua nini kinaendelea.
Alisema katika suala hilo, aliitwa na waandaaji kulizungumzia ambapo alikwenda akiwa na Rais wa bendi ya FM Academia, lakini akakuta wimbo wake umetolewa ndipo alipoona kuna ubabaishaji akaamua kujitoa kabisa na ndipo ulipoingizwa wimbo ya FM Academia.
Tuzo hizo pia zimewahi kususiwa na wasanii wa kizazi kipya kutokana na sababu kama za Choki kwamba kuna upendeleo katika utoaji wa tuzo hizo.
No comments:
Post a Comment