*Giraffe hoteli yatia mkono
Na Elizabeth Mayemba
KIKOSI cha Simba kinatarajia kuondoka kesho kwenda mjini Kigali, Rwanda kikiwa na msafara wa watu 40 kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho (CAF), dhidi ya Kiyovu ya huko, utakaopigwa Jumapili.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga alisema maandalizi kwa ajili ya safari hiyo yameshakamilika na wataondoka na ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda.
"Maandalizi kwa ajili ya safari hiyo yameshakamilika, hivyo utaondoka msafara wa watu 40, wachezaji, viongozi, benchi la ufundi pamoja na wadau wengine," alisema Kamwaga.
Alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mserbia Milovan Cirkovic, atatangaza kikosi kesho kutwa asubuhi, kwani kwa sasa hawezi kufanya hivyo kwa kuwa huenda kukatokea mabadiliko kwa mchezaji yeyote kuumia.
Pamoja na kutotaja kikosi, imefahamika kwamba kikosi kitakachokwenda Rwanda ni makipa Juma Kaseja na Ally Mstapha 'Bartez', Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Said Nassoro 'Chollo, Juma Jabu, Shomari Kapombe, Patrick Mafisango, Haruna Moshi 'Boban' na Mwinyi Kazimoto.
Wengine ni Salum Machaku, Edward Christopher, Ramadhan Singano, Gervais Kago, Rajab Isihaka, Uhuru Selemani, Felix Sunzu na Emmanuel Okwi.
Wachezaji ambao hawatakwenda kwa kuwa ni majeruhi ni Wilbert Mweta, Ulimboka Mwakingwe, Amir Maftah na Jonas Mkude.
Katika hatua nyingine, Hoteli ya Giraffe Ocean View imejitolea kuidhamini Simba katika mchezo wao wa marudiano dhidi ya Kiyovu, udhamini ambao utalenga malazi.
Ofisa Uhusiano ya hoteli hiyo, Elsie Mntenga alisema hoteli yake imejitolea kuidhamini Simba, ambapo watahusika zaidi na malazi kwa wageni.
No comments:
Post a Comment