17 February 2012

Tevez aja kivingine Man City

LONDON, Uingereza

CARLOS Tevez juzi alirejea katika timu yake ya Manchester City akitokea kwao Argentina akionekana kutokuwa na furaha huku akiwa amevaa jaketi lililoandikwa mgongoni 'Billionaire'.

Amerejea katika timu hiyo wakati karibuni alitoa lawama kwa Kocha Roberto Mancini kutomtendea vyema na kumchukulia kama mbwa.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun Kocha, Mancini amekanusha shutuma hizo kwa kusema: "Ninapingana na Carlos kwa ujumla na kile alichosema kwakuwa sijawahi kumtendea vibaya.

"Pengine ni kinyume chake na kila wakati nimekuwa nikimtendea vizuri.

"Lakini hilo limekwisha. Sitaki kulizungumzia zaidi. Hili ni swali la mwisho ninalojibu kuhusu yeye kwa miezi mitatu mingine."

Kuna kila dalili kwa Mancini kuwa tayari kumsamehe Tevez, ambaye anarejea katika klabu baada ya kupita miezi mitatu akiwa ameondoka klabuni bila kuaga, kutokana na kugoma kupasha mwili katika mchezo dhidi ya Bayern Munich.

Tevez akiwa katika uwanja wa mazoezi wa Carrington juzi alifanya mazoezi pekee yake wakati wachezaji wenzie waliondoka kwenda Ureno kwa ajili ya pambano lao la Ligi ya Europa dhidi ya Porto lililofanyika usiku wa kuamkia leo.

Wakati alipoulizwa kuhusu Tevez, Mancini  alisema: "Sitaki kujibu swali hili kwakuwa mchezo tunakwenda kucheza ni muhimu zaidi kuliko hili.

"Tuna mechi hii ambayo ni muhimu sana kwa kucheza dhidi ya timu kubwa ya Porto."

Chanzo cha karibu kilisema kuwa kocha huyo ni mtu wa kusamehe na atafungua mlango kwa Tevez kama tu atakuwa tayari kuomba msamaha ili kumaliza jambo hilo na kuanza tena kucheza, licha ya kwamba ameumizwa na kile alichosema(Tevez) mwishoni.


No comments:

Post a Comment