17 February 2012

Serikali yaunga mkono uchimbaji wa urani

MUhidin Amri na Joseph Mwambije, Ruvuma

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Gharib Mohamed Bilal  amewahakikishia wakazi wa mkoani Ruvuma kwamba utekelezaji wa uendeshaji wa Mgodi wa Urani mkoani humo utatekelezeka kwa wakati.

Alisema mradi huo ambao upo Wilaya ya Namtumbo mkoani humo utatekelezwa kwani una umuhimu mkubwa katika kukuza na kuendesha uchumi wa Taifa.

Hayo aliyasema jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa mgodi huo unaomilikiwa na Kampuni ya Mantra Tanzania wilayani humo.

Alisema, Serikali inafuatilia kwa makini kuona madini hayo muhimu yana wanufaisha Watanzania pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.

Dkt. Bilal aliongeza kuwa ana uhakika kuwa taratibu zote za hifadhi ya mazingira na usalama wa maisha ya wakazi wanaozunguka eneo hilo umetiliwa mkazo na kampuni husika kwa kushirikiana na Taasisi ya Nishati na Atomiki Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mantra Tanzania, Bw.Asa Mwaipopo aliiomba Serikali kuharakisha taratibu za kisheria zinachukuliwa ili mgodi uweze kuanza kufanya kazi mwakani.

"Na ifikiapo 2014 uzalishaji uanzae, ili ajira zipatazo 1,600 wakati wa ujenzi wa mgodi na zingine 400 wakati wa uzalishaji ziweze kupatikana kwa Watanzania na kusaidia kukuza uchumi," alisema

No comments:

Post a Comment