CHAMA cha Netiboli Tanzania (CHANETA) na kile cha Zanzibar (CHANEZA), vimekubaliana kuiingiza kambini timu ya taifa ya mchezo huo 'Taifa Queens', Februari 20 mwaka huu kujiandaa na michuano ya Afrika.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao cha pamoja kilichohusisha viongozi wa CHANETA na CHANEZA, kilichofanyika juzi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi alisema wamekubaliana kuita wachezaji 30 ambapo CHANEZA, itatoa wachezaji 10 na wao watatoa 20 ambao watakaa kambini jijini Dar es Salaam.
Alisema kambi hiyo ni maalumu kwa ajili ya michuano hiyo ya Afrika, ambapo Tanzania imepewa kibali na Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (IFNA), kuandaa mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika Mei 8 mwaka huu.
Rose alisema tayari wametuma barua kwa nchi zinazotakiwa kushiriki mashindano hayo, ambapo wanatarajia kupokea zaidi ya timu 16 kutoka nchi za Afrika.
Alisema mashindano hayo yataiwezesha Tanzania kupanda viwango vya IFNA, ambavyo kwa sasa inashika nafasi ya 22 duniani na nafasi ya tatu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katibu huyo alisema wameamua kuweka kambi ya wachezaji hao mapema, ili Taifa Queens iweze kufanya vizuri katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Kwa mara ya kwanza Tanzania iliandaa mashindano hayo mwaka 2009, na hii itakuwa mara ya pili kuandaa.
ends....
No comments:
Post a Comment