08 February 2012

Sunzu kuongeza 'chachandu' Simba

Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic amesema kupona kwa mshambuliaji wake Felix Sunzu, kutaisaidia timu yake katika mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Azam FC, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sunzu alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu, baada ya kuumia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Tusker ya Kenya na hivyo kukosa mechi tatu za ligi, ambazo ni Coastal Union, JKT Oljoro na Villa Squad.

Akizungumza kwa simu akiwa Bamba Beach Kigamboni nje kidogo ya Dar es Salaam, ambako timu yake imeweka kambi, Milovan alisema amefarijika kurudi uwanjani kwa Sunzu, kwani kutaongeza nguvu katika kikosi chake hasa kwenye mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Azam FC.

"Nimefurahi kuona Sunzu yupo fiti kabisa, hivyo ni imani yangu kubwa ataongeza nguvu katika mchezo wetu ujao dhidi ya Azam, kwani kila mtu anajua uwezo wa Sunzu," alisema Milovan.

Alisema Sunzu atasaidiana na mshambuliaji mwenzake Emmanuel Okwi kufanya mashambulizi ya nguvu, hasa kutokana na kiungo wake Haruna Moshi 'Boban' kuwa na kadi nyekundu hivyo kukosa mechi hiyo na nyingine inayokuja.

Boban alipewa kadi nyekundu, wakati timu yake ilipocheza na JKT Oljoro ambapo walishinda mabao 2-0, baada ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Oljoro, kadi yake ilianza kufanya kazi wakati timu yake ilipocheza na Villa, hivyo atakosa mechi nyingine mbili kwa sababu alipewa kadi nyekundu ya moja kwa moja.

Milovan alisema kiungo wake wa pembeni Ulimboka Mwakingwe, bado anasumbuliwa na nyonga hivyo yupo katika matibabu, lakini hali yake inaendelea vizuri kwa sasa.

No comments:

Post a Comment