08 February 2012

Yanga kazi nzito leo

*Kuua ndege wawili kwa jiwe moja
Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga leo itatupa karata yake nyingine katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara, itakapoikaribisha Mtibwa Sugar kwenye mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani wa aina yake kutokana na historia ya timu hizo kwa miaka ya hivi karibuni, ambapo Mtibwa imeonekana kuwa na matokeo mazuri kwa Yanga.

Katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Mtibwa iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakati huo Yanga ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Sam Timbe.

Ukiachilia mbali matokeo hayo, katika msimu uliopita Yanga iliambulia pointi moja kwenye mechi mbili za ligi walizokutana ambapo katika mechi ya kwanza, Yanga ililazimisha sare ya bao 1-1 na marudiano ililala kwa bao 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pamoja na hali hiyo, Yanga hivi sasa ipo katika hali ngumu katika kuhakikisha inatetea ubingwa wao, hasa baada ya kuonekana inayumbayumba katika baadhi ya mechi.

Katika mechi hiyo Yanga itapigana kufa au kupona, kuhakikisha wanalipiza kisasi pamoja na kuikamata Simba ambayo ndiyo vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 34 ikifuatiwa na Azam FC, yenye pointi 32 na Yanga ina pointi 31. Kwa kufanya hivyo Yanga, itakuwa kama kuua ndege wawili kwa jiwe moja.

Yanga kama itashinda kwa idadi kubwa ya mabao zaidi ya manne itaipiku, Simba na kukaa kileleni mwa ligi hiyo kitu ambacho kitaongeza nguvu na hamasa kwa mashabiki wao wakati wa kujiandaa na mechi dhidi ya Zamaleki.

Katika mechi hiyo, Yanga itawakosa Nurdin Bakari ambaye siku si nyingi ataondolewa plasta ngumu (POP) katika kidole chake pamoja na nahodha Shadrack Nsajigwa, ambaye anatumikia adhabu yake ya kuoneshwa kadi nyekundu ila kipa Yaw Berko, tayari ameshapona na anaweza kucheza mechi hiyo.

Mtibwa yenyewe itamkosa Kocha Msaidizi, Mecky Mexime pamoja na baadhi ya wachezaji waliofungiwa kwa madai kuihujumu timu hiyo kwa kupata vipigo viwili mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani wa Manungu.

Timu hiyo ilianza mzunguko huo kwa kufungwa na JKT Oljoro bao 1-0 na baadaye kufungwa tena na Coastal Union ya Tanga kwa idadi kama hiyo, hivyo uongozi uliamua kuwasimamisha watu hao.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Mtibwa, Tommy Olaba alikiri kuanza vibaya katika mzunguko huo lakini ana imani watafanya vizuri kwenye mechi zinazofuata kwani tatizo la kufanya vibaya wameshalibaini.

Mtibwa ikiibuka na ushindi katika mechi hiyo bado itabaki katika nafasi ya tano, licha ya kufikisha pointi 25 na Oljoro itaendelea kubaki katika nafasi ya nne ikiwa na pointi zake 26.

No comments:

Post a Comment