Okwi aipaisha kileleni*Boban alimwa 'red card'
Na Zahoro Mlanzi
MABAO mawili yaliyofungwa na Emmanuel Okwi, yaliifanya timu ya Simba izidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kuichapa JKT Oljoro mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pamoja na ushindi huo, lakini timu hiyo ilijikuta kuanzia dakika ya 43, ikicheza pungufu baada ya kiungo, Haruna Moshi 'Boban' kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi, James Mhagama kutoka Ruvuma kutokana na kumpiga kiwiko Omari Mtaki.
Kabla ya Boban kutolewa, mchezo kwa ujumla ulikuwa ni wa vurugu kwa pande zote mbili kutokana na wachezaji wa timu hizo kuchezeana kibabe huku wengine wakipigana viwiko vya siri siri ambavyo mwamuzi hakuviona.
Kutokana na ushindi huo, Simba sasa ina pointi 34 ikiiacha Yanga katika nafasi ya pili kwa pointi 31 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 29 na Oljoro imebaki katika nafasi ya nne kwa pointi 26.
Bao la kwanza la Okwi lilifungwa dakika ya 60, akimalizia pasi safi iliyopigwa na Uhuru Seleman ambaye katika mechi hiyo alicheza katika kiwango cha juu, aliunasa mpira uliokolewa kizembe na nahodha Ali Omari.
Zikiwa zimebaki dakika saba kipyenga cha mwisho kupulizwa, Okwi tena alizima ndoto za Oljoro walionekana kusaka bao la kusawazisha kwa udi na uvumba kwa kufunga bao la pili akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Seleman aliyeonana vema na Patrick Mafisango na kumpasia mfungaji.
Mechi hiyo ilikuwa na ushindani wa aina yake kwani katika dakika 30 za kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu lakini washambuliaji wa pande zote hawakuwa makini kufunga.
Dakika ya 31, Boban aliuwahi mpira uliopigwa na kipa, Juma Kaseja na kupiga shuti lililodakwa na kipa Said Lubawa akiwa ndani ya eneo la hatari.
Oljoro nayo ilijibu shambulizi hilo dakika ya 38 baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza ambapo Omari Khamis alipanda na kupiga krosi safi lakini ilikosa mmaliziaji na mashabiki kuanza kulaumu.
Kutokana na mechi ilivyoonekana ya kukamiana Boban bila kutarajia alijikuta akirudishia faulo aliyochezewa muda mfupi lakini mwamuzi hakuona, na kumpiga kiwiko Mtaki na kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Matukio hayo yaliendelea kuonekana kila wakati na kufanya mechi kukosa ladha ambapo baadhi ya wachezaji kama Kelvin Yondani wa Simba na Kalage Mgunda wa Oljoro walionekana wakiwa chini kwa nyakati tofauti wakishika sura zao kutokana na viwiko vya siri walivyopigwa.
Licha ya mechi kutawaliwa kwa wa fujo lakini mpaka dakika 90 zikimalizika, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Simba: Kaseja, Nassor Said, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Yondani, Jonas Gerald, Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisango, Gervais Kago/Okwi, Boban na Seleman/Ramadhan Singano.
Ciao.....
No comments:
Post a Comment