Na Zuhura Semkucha, Shinyanga
WANANCHI wanaoishi vijijini wameombwa kujitokeza kutoa maoni yao juu ya marekebisho yanayofanyika kwenye uundwaji wa Katiba Mpya ili iwe na usawa baina ya walionacho na wasiokuwa nacho.
Hayo yalielezwa jana na wananchi waliokuwa wakishiriki kwenye mdahalo ulioandaliwa na Muungano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Shinyanga (SHIMUNGONET) ambao ulifanyikia mjini humo.
Walisema, Katiba inayotumika kwa sasa ilikuwa imeundwa na watu 20 awali lakini umefika wakati wa kuunda wenyewe Katimba wanayoona ndiyo chaguo lao.
Mmoja wa wananchi hao, Bw.Sebastian Peter alisema, wananchi wote wana haki ya kutoa maoni katika kuunda Katiba Mpya ili kupata mtazamo wa Watanzania wote na kuweza kutetea haki yao.
“Kila mwananchi anatakiwa kutoa mchango wa kuchangia Katiba Mpya, tunatakiwa
tujitokeze tusiogope, halafu baadaye tukaanza kulalamika kuwa tunakandamizwa na katiba tuichangie sisi wenyewe na tunaomba washirikishwe watu wote mpaka huko vijijini,”alisema Bw.Peter.
Wakati huo huo wananchi hao walisema, Katiba inatakiwa izingatie wanyonge na maslahi ya wananchi wa kawaida pia mikataba iangaliwe upya ilenge kuwanufaisha wao na siyo kuwanufaisha wawekezaji na isiwe na mikataba ya muda mrefu.
Walisema, mikataba ya muda mrefu imekuwa ikiwaumiza hasa wale wanaoishi maeneo yanayozunguka migodi ya kemikali kwa madai kuwa huwa inawaharibu ngozi bila fidia yoyote.
“Mazingira tunayoishi ni magumu sana, jamani sheria ituangalie na sisi jamani, hali sio nzuri huko Serikali itukumbuke,” alisema mmoja wa wachangiajia hao ambaye alijitambulishwa kwa jina la Bw. Masunga.
No comments:
Post a Comment