03 February 2012

Balozi Seif aagiza mifuko ya jamii iwafikie wakulima

Na Queen Lema, Arusha

MAKAMU wa Pili wa Rais kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd ameiagiza mifuko ya kijamii nchini kuwekeza shughuli zake maeneo ya vijijini ili iweze kuwanufaisha wakulima katika vijiji mbalimbali.


Alisema hatua hiyo itasaidia kuwatatulia shida mbalimbali wakulima wadogo wadogo hasa kwa kujiwekea akiba endelevu.

Agizo hilo alilitoa jana jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa Mfuko wa Hifadhi ya Taifa (NSSF) ambao uliwakutanisha wadau mbalimbali jijini humo jana.

Balozi Seif alisema, kwa sasa asilimia kubwa ya wakulima hasa wa vijijini wanashindwa kufikia malengo yao mbalimbali kutokana na sababu tofauti tofauti zikiwemo kusahaulika na kampuni ama asasi ikiwemo mifuko kama hiyo.

Alisema, endapo mifuko hiyo ya kijamii itaweza kuboreshwa hata katika maeneo ya vijijini ni wazi kuwa wakulima wataweza kufanya kilimo chao kuwa cha ubora kwa kuwa watakuwa na akiba hususani kipindi cha uzeeni.

“Ni changamoto kwa taasisi mbalimbali, pamoja na mifuko kama hii, kuhakikisha wanawasaidia wakulima kwa kuwapa fursa mbalimbali za kujiunga na mifuko hii, kwa kuwa njia hii itaweza kuharakisha maendeleo ya vijiji na kilimo chenyewe,”alisema

Aliongeza kuwa wakulima hao kama wataweza kuhusishwa na mifuko hiyo basi hata kiwango cha wanachama nacho kitaweza kuongezeka kwa wingi kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wakulima hasa katika maeneo ya vijijini.

Balozi Seif alisema, mifuko mbalimbali hapa nchini inapaswa kuhakikisha inabuni na kuimarisha huduma zao ikiwa ni pamoja na kubuni miradi mbalimbali ambayo itasaidia kuongeza kiwango cha ajira na uchumi.

Alisema, mbinu hiyo itasadia kupunguzia matatizo mbalimbali ambayo yanaikabili Serikali hali ambayo nayo itakuwa ni chanzo kimoja wapo cha mafanikio nchini.

Katika hatua nyingine pia Balozi Seif alisema, ili mifuko hiyo ya kijamii iweze kufikia malengo yake mbalimbali ambayo wamejiwekea wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatafuta wabia katika nchi nyingine za Bara la Afrika, ambapo utaratibu huo nao utaweza kuwa na faida kwa jami

No comments:

Post a Comment