17 February 2012

Japan yatangaza neema Tanzania




 


 Balozi wa Japan nchini Tanzania, Bw.Masaki Okada akisoma hotuba wakati wa uzinduzi wa Zahanati ya Igoko mkoani Tabora juzi, kushoto ni Mkuu wa mkoa huo, Bi.Fatma Mwassa na Askofu wa Kanisa la Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Mhashamu Paul Ruzoka. Zahanati hiyo imefadhiliwa na Japan kupitia ubalozi wake nchini. (Na Ubalozi wa Japan)



Na Godfrey Ismaely, Dar es Salaam

BALOZI wa Japan nchini Tanzania, Bw.Masaki Okada amesema nchi yake ipo katika harakati mbalimbali za kuhakikisha inatoa michango yake katika sekta za afya ili kuhakikisha kuwa zinawahudumia Watanzania ipasavyo.

Alisema iwapo sekta za afya hususani zahanati, hospitali na vituo vingine vitajengewa uwezo wa kupatiwa vifaa vya kutosha ni dhairi kuwa huduma zilizotarajiwa zitapatikana kwa wakati.

Hayo aliyasema juzi katika sherehe za kufungua majengo ya Zahanati ya
Igoko iliyopo wilayani Uyui Mkoa wa Tabora ambayo ilikuwa chini ya ufadhili wa nchi hiyo kupitia ubalozi wake hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa jana na Ubalozi wa Japan kwa vyombo vya habari ilifafanua kuwa mbali na sherehe hizo kuudhuriwa na Balozi Okada pia Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bi. Fatma Mwassa, Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Bw. Stanley Kolimba na Mbunge wa Tabora Kaskazini, Bw.Sumar Mamlo walifanikiwa kuiwakilisha Serikali.

"Mabibi na mabwana, nina furaha sana kushiriki, kwenye hii sherehe ya kufungua majengo mapya kwenye zahanati hii ya Igoko. Nina furaha pia kufika Igoko Wilaya ya Uyui mkoani Tabora kwa mara ya kwanza;

"Nilipata taarifa kuwa maeneo mengi, pamoja na Igoko hakuna umeme wa TANESCO (Shirika la Umeme nchini), wala maji ya kutosha. Katika mazingira magumu kama haya ni matumaini yangu kuwa msaada wetu wa kuweka umeme wa 'Solar' (umeme wa jua) na tenki kubwa la maji vitasaida kuiendesha hii zahanati," alifafanua Balozi huyo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.
   
Hata hivyo taarifa hiyo ilifafanua kuwa mradi huo ambao ulikuwa ni ombi la Kanisa la Katoliki Dayosisi ya Tabora, nchi ya Japan iliweza kujitolea zaidi ya dola za Kimarekani 106,341 kwa lengo la kukamilisha upanuzi wa zahanati hiyo kupitia Mpango wa Ruzuku kwa Kuziwezesha Huduma Mbalimbali za Kijami kupitia nchi wahisani wa nchi hiyo (GGHSP).

"Kama sehemu ya kutimiza wajibu wa kuijengea jamii uwezo, Kampuni ya Kijapan ya Sumitono Chemical nayo imetangaza kutoa vyandarua 40 aina ya 'Olyset Net' ili kuzuia mbu waenezao Malaria katika Zahanati ya Igoko," alisema.

Balozi Okada aliongeza kuwa Serikali ya Japan itaendelea kuongeza nguvu katika huduma mbalimbali za kijamii hususani afya, elimu na upatikanaji wa maji kupitia mpango wa GGHSP.

No comments:

Post a Comment