Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam,Bw. Said Meck Sadiq, amezipongeza sekondari zilizofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2011 mkoani humo na kuzionya zilizofanya vibaya akitaka zijirekebishe.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Bw. Sadiq alisema kuwa ni jambo la kujivunia kuona kuwa shule za mkoa huo zimefanya vizuri na kushika nafasi za juu kitaifa pamoja na wanafunzi akizipongeza pia zilizofanya vema kimkoa.
“Nawapongeza waliofanya vizuri, kwa waliofanya vibaya nawaonya wajirekebishe, wachunge nidhamu za walimu katika ufundishaji hata za wanafunzi,”alisema Bw. Sadiq.
Katika matokeo yaliyotangazwa juma lililopita na Baraza la Mitihani la Taifa yalionesha kuwa katika shule zilizokuwa na watahiniwa zaidi ya 40 kitaifa Sekondari ya Fedha Boys ilishika nafasi ya pili, St Joseph Millenium nafasi ya tatu na Cannossa nafasi ya nane.
Matokeo hayo kwa Kanda ya Dar es Salaam yanaonesha kuwa Sekondari ya Thomas Moore ilishika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Feza Girls ambapo Sekondari ya Lilian Kibo imeshika nafasi ya tatu baada ya kufanya mtihani huo kwa mara ya kwanza.
“Kwa shule hiyo iliyofanya mtihani huo kwa mara ya kwanza na kushika nafasi ya tatu kimkoa hiyo ni matokeo mazuri nawapongeza, na waendelee hivyo,” alisema
Mbali ya kushika nafasi ya tatu kimkoa, Sekondari ya Lilian Kibo imeshika nafasi ya 15 kitaifa, ambapo pia imeshika nafasi ya tatu kimkoa katika somo la Jiografia na ya 11 kitaifa
Shule hiyo pia imekuwa ya tisa kitaifa katika somo la utunzaji wa hesabu(accounts) na ya sita kimkoa huku ikishika nafasi ya 10 kwa hisabati, historia nafasi ya sita, fizikia nafasi ya 9 na kemia nafasi ya 7 kimkoa.
No comments:
Post a Comment