Na Yusuph Mussa, Kilindi
KATIKA ukurasa wa 18 wa gazeti hili kuna habari kuhusu madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi,Mkoa wa Tanga kupitisha azimio la kuwafikisha mahakamani wakuu wa idara 11 ili kujibu mashtaka ya ubadhirifu wa fedha za umma.
Madiwani hao walipitisha uamuzi huo baada ya kukaa kama Kamati ya Fedha na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa pamoja waliridhia huo uliofanyika kati ya mwaka 2008-2009. Akisoma uamuzi huo mmoja wa diwani huyo aliwataja viongozi wote ambao watachukuliwa hatua za kisheria, kinidhamu na wale ambao watatakiwa kurejesha fedha zilizoibwa.
Fedha ambazo zilifanyiwa ubadhiri za miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, mfuko wa barabara, kilimo, maji, fedha za ununuzi wa power tillers (pembejeo) na utawala na mishahara.
Kwanza tunawapongeza madiwani hao kwa kuonesha kukerwa na matumizi mabaya ya fedha za umma hivyo kuagiza waliohusika kufikishwa mahakamani. Tunaunga mkono uamuzi huo hasa kwa kuzingatia watendaji wengi kwenye halmashauri na manispaa wanatumia vibaya madaraka yao.
Watendaji wa aina hiyo ndio wanaosababisha halmashauri na manispaa kupata hati chafu, matokeo yake kusababisha halmashauri hizo kunyimwa fedha za ruzuku.
Kwa hili tuna kila sababu ya kuwapongeza madiwani wa Kilindi na kinachotakiwa sasa hatua walizopendekeza zichukuliwe mara moja. Haiwezekani watu wachache wajineemeshe kwa fedha za umma huku miradi mingi ya kuwakomboa wananchi kiuchumi ikikwama.
Uamuzi wa madiwani hao ndiyo njia pekee ya kupambana na watumishi waliogeuka mchwa kwenye halmashauri kwa kutafuna mamilioni ya fedha za miradi.
Tuna kila sababu ya kuunga mkono ujasiri wa madiwani hao kwani kwa kufanya hivyo wanaunga mkono jitihada za Rais Jakaya Kikwete za kuhakikisha watumishi hao wanang'olewa.
Tunawapongeza madiwani kwa kuingia kwenye vita hii. Tunasema huo ndiyo uwakilishi kwani wajibu wao ni pamoja na kuona raslimali za wananchi zinatunzwa.
Kwa msingi huo madiwani wa halmashauri zingine nchini wanatakiwa wajifunze kwa wenzao wa Kilindi. Kamwe tusikubali watumishi wachache wageuze nchi yetu shamba la bibi.
No comments:
Post a Comment