03 February 2012

RC awashauri wabunge

kuwadhamini wakulima

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MWITO umetolewa kwa wabunge na watu wenye uwezo kutumia nafasi zao kwa ajili ya kuwadhamini wakulima ambao wako tayari kukopa zana za kilimo ili kuendeleza kilimo nchini.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dkt. Rehema Nchimbi alitoa wito huo jana wakati akikabidhi matreka madogo (power tiller) 10 kwa wakulima wa wilaya ya Mpwapwa ambao walifadhiliwa na Mbunge wa Kibakwe, Bw.George Simbachawene.

Dkt.Nchimbi alisema, kama wafanyabiashara na watu wenye uwezo wataamua kwa dhati kusimamia na kuwahamasisha wakulima kukopa matrekta na pembejeo, ni dhahiri kuwa baada ya muda mfupi suala la njaa mkoani Dodoma litakuwa ni hadithi.

“Haiwezekani mnapanga kila wakati kwamba mnataka kuwapa samaki, hebu badilikeni basi muwape ndoana, kama alivyofanya Simbachawene mbona inawezekana jamani," alisema Dkt.Nchimbi.

Mkuu huyo aliwata wakulima kutoogopa kukopa matrekta kwani masharti yake ni nafuu ukilinganisha na mikopo mingine kutoka taasisi zinazokopesha kama  benki ambazo zimekuwa zikitoza riba kubwa.

Alisema, Mkoa wa Dodoma unabahati ya pekee kwa kutengewa kituo cha kuuzia zana hizo chini ya wakala wa Sinana Inteprises ambao ni wakala wa SUMAJKT kwani ipo mikoa ambayo wanatafuta nafasi za kupata kama Dodoma lakini hawajapata.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Bw.Simbachawene alisema, aliguswa kwa kuona kuwa upo umuhimu wa kutoa udhamini kwa wapiga kura wake ambao wako tayari kwa ajili ya kilimo ili waweze kujimboa.

Mbunge huyo alisema, uamuzi wake huo utakuwa ni wa kudumu kutokana na ukweli kuwa ana imani kwa wakulima katika kuzitumia vema zana hizo na akawataka na wengine katika jimbo lake kujitokeza zaidi.

Hata hivyo alilalamikia bei kubwa wanayotoza katika vifaa hivyo ambayo alisema, hailingani kabisa na bei ya soko na kwmaba hiyo ni sababu mojawapo ya kuwakimbiza wakulima na kuwafanya waogope hata kununua au kukopa vifaa hivyo.

“Mheshimiwa Mkuu, lazima jambo hili liangaliwe kwa mapana hivi ni wapi bei inakuwa kubwa zaidi maana kama hizi power tiller 10 leo (jana) tumezinunua kwa zaidi ya shilingi milioni 84, hii ni bei kubwa mno, Mkuu fanyeni uchunguzi wa kujua ni wapi bei inapoongezeka," alifafanua Bw. Simbachawene.

No comments:

Post a Comment