Na Joseph Mwambije, Ruvuma
BALOZI wa Cuba nchini, Bw. Ernesto Gomez Diaz amesema uhusiano wa nchi yake na Tanzania ni wa muda mrefu na utaendelea kudumishwa kwa kuwekeza katika fursa mbalimbali za uchumi.
Balozi huyo aliyasema hayo jana mkoani Ruvuma wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo baada ya kufanya ziara ya kikazi, mazungumzo ambayo yalifanyikia katika ofisi ya Mkuu wa mkoa.
‘Uhusiano wetu ulikuwepo tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere, huku Tanzania ikifuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, wakati nchi yetu ni ya Kikomunisti sawa na China ikiwemo Korea Kusini, hivyo miaka ya nyuma tuliwekewa vikwazo na Marekani, lakini tukavuka vikwazo hivyo na tunasonga mbele," alisema
Alisema, nchi yake imepiga hatua katika masuala ya afya na madaktari wake wamesambaa duniani wakitoa huduma za afya na kwamba nchi hiyo inatoa elimu ya afya bure kuanzia ngazi ya chini hadi Chuo Kikuu.
Balozi huyo alisema, nchi yake yenye wakazi milioni 12 ina madaktari 80,000 na imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania katika sekta ya afya ambapo kuna madaktari wa nchi hiyo wanaofanya kazi nchini ukiwemo mkoa huo ambao una madaktari watatu kutoka Cuba.
Mbali na hayo Balozi huyo aliahidi kuongeza idadi ya madaktari nchini ambapo alifafanua kuwa kwa upande wa miradi nchi yake inafadhili mradi wa kujikinga na malaria na wana mpango wa kuifadhili Serikali ya Tanzania kupitia utokomezaji wa ugomjwa huo kupitia ujenzi wa kiwanda cha kuulia mazalia ya mbu.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt.Anselm Tarimo alisema, uhusiano huo utaendelea kudumishwa milele na kufafanua kuwa Tanzania kwa mara ya kwanza ilipokea madaktari kutoka Cuba mwaka 1980.
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji mkoani humo, Dkt.Hassan Lumbe alisema, ni jambo la faraja kupata madaktari toka Cuba kwa Mkoa wa Ruvuma ambao uko pembezoni na kubainisha kuwa kila baada ya miaka miwili wanapata madaktari toka nchi hiyo
No comments:
Post a Comment