Na Rehema Mohamed
KAMPUNI ya utalii, Omani Adventures ya nchini Oman imeahidi kuungana na Bodi ya Utalii ya Tanzania (TTB) kwa lengo la kuuza utalii wa Tanzania nchini Omani.
Ujumbe wa watalii sita ulioingia nchini mwishoni mwa wiki ulisema jukumu lao kubwa litakuwa ni kuisaidia serikali ya Tanzania kuongeza idadi ya watalii kutoka Omani kutembelea vivutio vya utalii nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, kiongozi wa watalii hao, Bw. Majid Abdullah Al Anboon, alisema wamevutiwa sana na vivutio vya utalii nchini na wako tayari kusaidia kuutangaza vivutio hivyo nchini kwao.
Alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi yenye vivutio vya kuvutia vya utalii ambapo aliahidi kuungana na Serikali katika kukuza uelewa wa vivutio hivyo nchi za nje.
“Haya yamekuwa matembezi ya historia kwetu, tumetembelea Bonde la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Tanganyika na Mlima Kilimanjaro. Maeneo yote yana mvuto wa kipekee,” alisema.
“Tutakuwa mabalozi wazuri nchini Omani, tutajitahidi kusambaza taarifa tulizokusanya katika matembezi yetu ambazo ni pamoja na picha, video na vipeperushi tulivyopokea kutoka bodi ya utalii Tanzania kwenye vyombo vya habari nchini na kuhamasisha watu wa Omani watembelee Tanzania ili kujionea mali za asili nzuri zilizopo nchini,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii ya Tanzania (TTB), Bi. Devota Mdachi, alisema kuwa ujio wa watalii nchini pamoja na ushirikiano walioahidi itakuwa chachu ya ongezeko la watalii kutoka Oman na kwingineko duniani.
“Tunafuraha kuwa watalii kutoka Omani wameahidi kutusaidia katika kutangaza utalii wetu kimataifa. Mpango wetu ni kuona watalii wengi zaidi wanakuja Tanzania,” alisisitiza.
Aliongeza kwamba pamoja na msaada wa Balozi wa Tanzania nchini Omani, bodi ya utalii itaongeza jitihada za kuhakikisha mahusiano mazuri na imara yanakua kati ya nchi hizo mbili ambayo yatawezesha kukua kwa sekta ya utalii ya nchi zote mbili.
Kwa upande wake, Meneja Masoko wa TTB, Bw.Geofrey Meena aliwaasa watalii wa Omani hao kujenja tabia endelevu ya kila mwaka kutembelea Tanzania katika kudumisha mahusiano baina ya pande mbili husika.
No comments:
Post a Comment