13 February 2012

Madiwani Mwanga wakosa imani na vyombo vya dola

Na Martha Fataely, Mwanga

BAZARA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, limesema vyombo vya dola wilayani humo
vimeshindwa kudhibiti uharibu mkubwa wa mazingira katika Mlima Kamwala unaotokana na uchomaji moto, uchomaji mkaa, uvunaji magogo na ukataji mbao.

Kutokana na hali hiyo, baraza hilo limedai kutokuwa na imani na vyombo hivyo hivyo kulazimika kuunda kikosi maalumu ambacho kitakwenda kumuona Mkuu wa Mkoa huo Bw. Leonidas Gama, ili kuomba msaada zaidi.

Kikosi hicho kinahusisha watu wanne kikiongozwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bi. Theresia Msuya, Mkurugenzi Bw. Willy Njau, Diwani wa Kata ya Mwaniko, Bw. Baraka Maradona Bw. Ashrafal Mruma wa Kata ya Mwanga Mjini.

Akizungumza katika kikao cha baraza hilo mwishoni mwa wiki, Bi. Msuya alisema vyombo hivyo vimeonesha udhaifu mkubwa katika kushughulikia tatizo la uharibifu wa mazingira katika mlima huo ambao unazungukwa na Kata za Shighatin, Ngujini, Kighare na Chomvu.

“Ofisa Maliasili wa Wilaya, Bi. Anjelina Sampa, amekuwa akipewa vitisho na wahalifu, ndani ya eneo la mlima kuna kiwanda cha kuzalisha pombe haramu ya gongo, kuna watu wanachoma mkaa na wengine wameweka makazi, jambo la kusikitisha pamoja na polisi kupewa taarifa, hakuna hatua zinazochukuliwa,” alisema.

Aliongeza kuwa, pamoja na vyombo hivyo kupewa orodha ya watu wanaoharibu mazingira kwa makusudi, hadi sasa wameshindwa hawajachukuliwa hatua zozote.

Bi. Msuya alisema mara kadhaa halmashauri imekuwa ikitumia askari mgambo kuwakamata wahusika lakini baadae waliwasaliti hivyo walilazimika kutumia Jeshi la Polisi ambalo nalo limeshindwa kazi hivyo wakalifikisha suala hilo kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ambayo pia imeshindwa kuchukua hatua.

diwani wa Kata ya Shighatin Bw. Enea Mrutu alisema anao ushahidi wa ujumbe mfupi wa maandishi juu ya kuendelea kwa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watumishi wa maliasili jambo ambalo linaashiria kuwalinda wahusika.

Alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Athuman Mdoe ambaye amekosa ushirikiano wa kutosha kutoka wasaidizi wake na kusababisha udhibiti wa suala hilo kuwa mgumu.

Alisema kutokana na hali, Bw. Gama ndiye kiongozi pekee anayeweza kudhibiti uharibifu huo kutokana na uadilifu ambao ameuonesha katika kipindi kifupi alichokaa mkoani hapa.

Kwa upande wake, Bw. Mrutu alisema ipo orodha ya wafanyabiashara wakubwa wanne wilayani humo ambao ndiyo vinara wa uharibifu wa mazingira na wameajiri watu wa kuchoma mkaa wakichukua vibali mkoani Tanga lakini hawashughulikiwi.

Awali diwani wa Kata ya Mwaniko, Bw. Maradona, alisema wananchi wa kata yake walikamata mbao zaidi 500 zilizovunwa kinyume cha sheria lakini zilizofikishwa wilayani ni mbao 300 huku nyingine zikiwa hazijulikani zilipo.




No comments:

Post a Comment