13 February 2012

Mwape anogesha 'Bithday' Yanga

*Afunga bao pekee *Simba bado ipo juu

Na Speciroza Joseph

BAO lililofungwa dakika ya 46 na mshambuliaji Davis Mwape liliifanya Yanga kusheherehekea miaka 77 kwa furaha tangu kuanzishwa kwake baada ya kuifunga Ruvu Shooting bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Kwa ushindi huo, Yanga imewiana na Simba kwa pointi zote zina pointi 37 ila Simba bado inaongoza ligi kwa tofauti ya bao moja na kuifanya Yanga ibaki nafasi ya pili.

Kabla ya kuanza kwa mechi hiyo ya jana ambayo ilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kulitanguliwa na mechi ya Yanga Veteran iliyoumana na Cloud's Media ambapo Yanga Veteran ilishinda bao 1-0.

Bao hilo pekee la Yanga Veteran lilifungwa na Ali Yusuph Tigana.

Katika mechi ya Yanga na Ruvu, timu zote zilianza kwa kasi na kushambuliana kwa zamu ambapo kwa upande wa Yanga iliongozwa na Mwape na Kenneth Asamoah na Ruvu iliongozwa na Mohamed Kijuso.

Dakika ya 29, Yanga ilipata penalti iliyotokana na Mwape kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Idd Nyambuso na mwamuzi Nathan Lazaro aliamuru ipigwe penalti ambayo ilipigwa na Hamis Kiiza lakini kipa Benjamin Hengu aliipangua na kutoka nje.

Ruvu nayo ilijibu mapigo dakika ya 32 kupitia kwa Kijuso ambaye alibaki na kipa Shaaban Kado lakini alishindwa kukwamisha mpira wavuni kwa shuti lake kutoka nje.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga ilifanya shambulizi la kushtukiza na katika harakati za kuokoa, mabeki wa Ruvu walimpasia Mwape ambaye alipiga shuti lililogonga mtamba wa panya na kutinga wavuni.

Baada ya kufunga bao hilo Yanga ilionekana kuridhika kwa kucheza kwa kujiamini huku ikipiga pasi nyingi lakini Ruvu yenyewe ilikuwa ikisaka bao kwa udi na uvumba.

Dakika ya 71, Ruvu inapata faulo iliyopigwa na Bakari Japher lakini kipa Kado aliokoa na mabeki kuondosha hatari na dakika ya 74, Seif Abdallah alishindwa kufunga bao pia alipobaki na kipa Kado kwa shuti lake kutoka nje.

Ruvu iliendelea kuliandama lango la Yanga lakini mpaka kipyenga cha mwisho kikipulizwa Yanga ilitoka kifua mbele kwa bao 1-0.

Yanga:Kado, Ibrahim Job, Stephano Mwasika, Nadir Haroub 'Canavaro', Athuman Idd 'Chuji', Juma Seif 'Kijiko', Omega Seme/Shamte Ally, Haruna Niyonzima, Mwape, Asamoah/Jeryson Tegete na Kiiza.




No comments:

Post a Comment