10 February 2012

Nyoni, Dkt.Mtasiwa wasimamishwa kazi

*Pinda asema Dkt. Mponda, Nkya nao kuchunguzwa
*Madaktari waipongeza serikali, wakubali kurudi kazini
*Wahadharisha madai yao kusikilizwa kabla ya Machi 3

Grace Ndossa na Rehema Maigala

SIKU moja baada ya wanaharakati jijini Dar es Salaam kuandamana kwa lengo la kuishinikiza Serikali ikutane na madaktari ili kuepusha vifo vya Watanzania wasio na hatia, Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, jana amewasimamisha kazi vigogo wawili wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Vigogo hao ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Deo Mtasiwa.

Bw. Pinda alitangaza uamuzi huo Dar es Salaam jana alipokutana na madaktari waliokuwa kwenye mgomo pamoja na wauguzi ambao walipokea uamuzi huo kwa shangwe na furaha kubwa.

Kutokana na tamko hilo, madaktari hao waliahidi kurudi kazini kuanzia leo ili kuokoa maisha ya Watanzania wanaoteseka kutokana na kukosa matibabu tangu mgomo huo ulipoanza.

“Hatua stahiki zimechukuliwa kwa mambo yanayozungumziwa wizarani hivyo Katibu Mkuu (Bi. Nyoni) na Mganga Mkuu wa Serikali (Dkt. Mtasiwa), tunawapa barua za kuachia ngazi, lengo ni kutoa nafasi ya kufanya uchunguzi, kusafisha Wizara na jina lake.

“Najua wataumia sana na kusema wameonewa, lakini hakuna jinsi, lazima waondoke ili kupisha uchunguzi na kusafisha jina la Wizara hii ambalo limechafuka sana,” alisema Bw. Pinda.

Madaktari na wauguzi ambao walikuwa makini kumsikiliza Bw. Pinda akitoa tamko hilo, walionesha furaha zao kwa kupiga kelele, miluzi na kugonga meza hali ambayo ilisababisha kiongozi huyo kusitisha hotuba yake kwa muda.

Habari za uhakika kutoka wizarani zinasema kuwa, watumishi wa Wizara hiyo wamefurahishwa na hatua ya Serikali kumsimamisha Bi. Nyoni kwa sababu wanazojua wenyewe.

Akizungumzia hatma ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hadji Mponda na Naibu wake, Dkt. Lucy Nkya, Bw. Pinda alisema, viongozi hao wana kofia ya kisiasa lakini watachunguzwa.

“Madaktari wangu chonde chonde, naomba mrudi kazini mkatumikie Watanzania, muwe na uzalendo na mzingatie viapo vyenu na moyo wa huruma,” Bw. Pinda aliwasihi madaktari hao.

Alisema Serikali inashughulikia madai yao tume iliyoundwa kupitia madai yao, imepewa siku 14 na kupeleka majibu serikalini ili kuona utaraibu wa kuongeza posho.


Kuhusu madai kuwa viongozi wanatibiwa nje ya nchi hata kwa magonjwa ambayo yanawezekana nchini, Bw. Pinda alisema kuanzia sasa watu wa ngazi ya chini ambao hawana uwezo ndiyo watapewa kipaumbele.

Akizungumzia hatua ya Serikali kupeleka baadhi ya viongozi kutibiwa nje ya nchi, Bw. Pinda alisema kuanzia sasa watalazimika kupimwa na madaktari watatu ili wajiridhishe kama kuna sababu za msingi za kupelekwa huko.

Aliagiza madaktari wote waliowahi kupewa vimemo na viongozi ili waruhusu wagonjwa fulani kwenda kutibiwa nje, waviwasilishe kwake ili hatua zaidi zichukuliwe.

“Madaktari zingatieni maadili ya kazi yenu si kukubali vimemo vinginevyo mtafanya biashara ya wagonjwa,” alisema Bw. Pinda na kuongeza kuwa, suala la kukopeshwa magari, wataingizwa katika utaratibu wa kukopeshwa vyombo hivyo vya usafiri.

Kuhusu nyumba za kuishi, alisema Serikali itawapa posho ili kulipia nyumba kupitia mishahara yao au kushirikiana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya kuwajengea nyumba.

“Hakuna daktari hata mmoja ambaye atafukuzwa kwa sababu ya kushiriki mgomo huu, endeleeni na kazi kwa amani na kuwaonesha upendo wagonjwa,” alisema.

Baada ya kumalizika hotuba yake, madaktari hao walimuhakikishia Bw. Pinda kuanza kazi rasmi kuanzia leo na kuitaka Serikali itekeleze ahadi yake.

Walisema kama Serikali itashindwa kufanyia kazi madai yao kabla ya Machi 3 mwaka huu, wataamua hatua zingine za kuchukua ambazo zitakuwa ni kali zaidi.

“Kabla ya sisi kurejea kazini, tunaomba wanaharakati wote waliokamatwa na polisi leo wakiwa katika majengo ya Hospitali hii ya Muhimbili kwa lengo la kututetea, waachiwe huru bila kuwekewa pingamizi lolote,” walisema.

Mwisho.

1 comment:

  1. Inabidi Pinda ujifukuze kazi wewe mwenyewe kwanza kwa sababu tayari mwanzo ulishatoa kauli kwa kusema kuwa madaktari wote wasiporudi kazini watakuwa wamefukuzwa kazi. Sasa mbona unakuwa na kauli mbili mbili na kuwa kigeugeu? Ulishachemsha kwa hiyo ni bora ukaondoka wewe.

    ReplyDelete