*Kura 361 zampa ushindi wa kuwania ubunge Arumeru
*CCM yatamba kuishangaza CHADEMA kama Igunga
*Uchaguzi huo watabiliwa kuwa na upinzani mkali
Na Queen Lema, Meru
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, kimemteua Bw. Solomoni Sumari, ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Jeremiah Sumari kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika Aprili mosi mwaka huu.
Bw. Sumari aliibuka mshindi katika kura za maoni ili kupata mgombea ambaye atakiwakilisha chama hicho katika uchaguzi huo na kuwashinda wenzake watano waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ambapo matokeo hayo yalitangazwa juzi jioni.
Msimamizi kura hizo Bw. Saimon Saningo, alisema Bw. Sumari alipata kura 361 wakati mpinzania wake mkubwa, Bw. William Sarakikya, akipata kura 359.
Wagombea wengine na kura zao kwenye maabano ni Bw. Elishilia Kaaya (176), Bi. Elirehema Kaaya (205), Bw. Rishankira Urio (11), na Bw. Anthony Musani (22).
“Kwa mamlaka niliyonayo, namtangaza Bw. Solomoni Sumari kuwa mshindi wa kura hizi ambaye atakiwakilisha chama chetu katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki, idadi ya kura zote zilizopigwa ni 1,034,” alisema Bw. Saningo.
Aliwataka wagombea walioshindwa, wasikate tamaa badala yake washirikiane na mgombea aliyeshinda kuhakikisha jimbo hilo halichukuliwi na wapinzani kama ilivyokuwa katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, mkoani Tabora.
“Wagombea mlioshindwa, nawaomba mumpe ushirikiano Bw. Sumari ambaye ndiye mshindi wa kura za maoni, hakikisheni nguvu mliyoitumia kuomba nafasi hii, inatumika kutetea jimbo hili lisiende upinzani wakati wa kampeni,” alisema.
Aliongeza kuwa, kama kiti hicho kitatetewa vizuri na wagombea walioshindwa katika kura za maoni, jimbo hilo litaendelea kuwa chini ya CCM ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Hadi sasa, chama kingine cha siasa ambacho kimetangaza kusimamisha mgombea wake katika uchaguzi huo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Uchaguzi huo unatabiriwa kuwa na ushindani mkubwa kati ya mgombea wa CCM na CHADEMA ambacho tayari kimeanza ziara ya kuimarisha chama hicho mkoani Tanga.
Tunawatakia kampeni za amani bila rafu apatikane mbunge aliyepitishwa na watu na sio pesa wala wizi wa kura wala ubabe
ReplyDelete