23 February 2012

Mapato yazua balaa Yanga

*Bhinda kujadiliwa, Ofisa Tawala asimamishwa

Na Elizabeth Mayemba

SAKATA la mapato ya mechi ya Klabu Bingwa Afrika, kati ya Yanga na Zamalek ya Misri yamezua balaa, baada ya uongozi wa klabu hiyo kutoana kafara kuhusiana na suala hilo.

Viongozi waliokumbwa na mshikemshike huo ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Mohamed Bhinda, ambaye atajadiliwa kuhusiana na sakata hilo la mapato huku Ofisa Tawala wa klabu hiyo, Masoud Sad akiwa amesimamishwa.

Katika sakata hilo, Mhazini wa klabu hiyo, Philipo Chifupa naye amepewa onyo huku akiendelea kuchunguzwa mwenendo wake na uongozi wa klabu hiyo.

Mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa ilichezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Pia wengine wanaotuhumiwa na sakata hilo ni Mhazini wake Philipo Chifuka pamoja na mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, ambaye pia ananyadhifa nyingine, viongozi hao wawili mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni haikufahamika kama nao wamesimamishwa.

Habari za uhakika zilizopatikana Dar es Salaam jana kutoka ndani ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Yanga, zilidai kwamba viongozi hao walichukua baadhi ya tiketi kutoka mwa uongozi wa Kampuni ya Prime Time Promotions, ambayo ilipewa mamlaka ya kusimamia mauzo ya mechi hiyo.

Hata hivyo chanzo hicho kilieleza kwamba licha ya kutoana kafara, wajumbe wa kamati hiyo walihoji iweje watu wa chini wafanye maamuzi bila uongozi wa juu kufahamishwa kinachoendelea.

"Viongozi hao walichukua tiketi kwa madai kwamba shughuli iliyokuwa ikifanywa na Prime Time Promotions, ilikuwa haiendi vizuri," kilidai chanzo hicho.

Chanzo hicho kilieleza kwamba kutokana na hali hiyo baadhi ya viongozi wa Yanga, waliiomba Prime Time Promotions iwape ufafanuzi wa kutosha na kuwataja waliochukua tiketi hizo.

Ilidaiwa kiasi cha mapato kilichotangazwa ni kidogo, tofauti na mapato yaliyopatikana na cha kushangaza zaidi wakati wa kutangaza mapato kulikuwa na hali ya kusuasua.

"Hata hivyo tayari Kamishna wa mechi hiyo kutoka Malawi, alishakabidhiwa na kuyatuma kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), ambapo inadaiwa kiasi cha mapato kilichotangazwa hakikuwa sahihi," kilidai chanzo hicho.

Hata hivyo juzi taarifa zilizofika kwenye vyombo vya habari ilidaiwa kuwa mechi hiyo iliingiza kiasi cha sh.milioni 289 kutokana na mashabiki 43,495 walioingia uwanjani.

Alipotafutwa Bhinda kuzungumzia sakata hilo, Bhinda alisema hajapata taarifa ya kujadiliwa hivyo anasubiri kujulishwa ili na yeye atolee ufafanuzi kwa kuwa yeye aliyekuwa mmoja wa waratibu wa mechi kwa upande wa Yanga. 


No comments:

Post a Comment