*Jaji akwamisha kesi ya Kafulila, sasa kusikilizwa Machi 15
*Kesi ya Mbowe, Dkt. Slaa kusikilizwa leo mjini Arusha
Zourha Malisa na Zena Mohamed
MBUNGE wa Wawi, Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Hamad Rashid Mohammed, amesema hana mpango wa kuanzisha chama kipya cha siasa kama inavyodaiwa bali ataendelea kuwa mwanachama wa chama hicho.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu jana, Bw. Mohammed alisema kuwa, hawezi kuanzisha chama kingine cha siasa kwa sababu kesi yake ya msingi, ipo mahakamani.
“Mimi ni mwanachama hai wa CUF, ndio maana hadi sasa kesi ya msingi ipo mahakamani, napigania haki yangu nikiwa kama mwanachama wa CUF, si vinginevyo, suala la kuanzisha chama kingine cha siasa haliwezekani.
“Tusubiri mahakama itoe uamuzi wake baada ya hapo ndio tutajua mwelekeo ni upi, nasikia kuna chama kimeanzishwa na baadhi ya wanachama waliojitoa CUF, lakila si mimi,” alisema Bw. Mohammed na kusisitiza msimamo wa kupigania haki yake.
Tangu chama hicho kikumbwe na migogoro, kumekuwa na tetesi zinazosema Bw. Mohammed ana mpango wa kuanzisha chama cha siasa kinachotajwa kwa jina la ADC.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Mkurugenzi wa Maadili wa CUF Taifa, Bw. Abdallah Kambaya, alisema lengo la watu wanaohama CUF ni kuanzisha chama kipya si kwa ajili ya kuiondoa CCM, bali kukimaliza chama hicho.
“Kuanzisha chama kingine si kigezo kuwa CUF itakufa, haiwezi kufa kwa ajili ya kuanzisha vyama vidogo ambavyo havina tija yoyote kwa Taifa hili,” alisema, Bw. Kambaya.
Wakati huo huo, Rehema Mohamed anaripoti kuwa, mashauri ya kesi za mauaji yanayoendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Morogoro, yamesababisha kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama iliyofunguliwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila, na wenzake, dhidi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, ihairishwe.
Kesi hiyo ilikuwa itajwe jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ili kupangiwa tarehe ya kusikilizwa lakini ilihairishwa baada ya jaji aliyepangwa kusikiliza shauri hilo Alis Chinguwile, kuwa mkoani Morogoro akisikiliza kesi za mauaji zinazokabili watuhumiwa mbalimbali.
Msajili wa Mahakama Kuu, Bw. Amir Msumi, aliziambia pande zinazohusika kuwa, Jaji Chinguwile, yupo Morogoro kwa ajili ya kusikiliza mashauri ya kesi za mauaji, hivyo imepangwa kusikilizwa Machi 15 mwaka huu.
Katika kesi ya msingi Bw. Kafulila kupitia mawakili wake, anapinga uamuzi wa chama hicho kumvua uanachama akidai haukuwa halali kwa sababu Katiba ya chama hicho haikufuatwa.
Madai mengine ni kutopewa haki ya kusikilizwa licha ya kwamba ni haki yake ya msingi. Anadai kuwa, wajumbe walioshiriki kupitisha uamuzi huo, wengine hawakuwa wajumbe halali.
Uamuzi wa kumfukuza uanachama Bw. Kafulila na wanachama wengine sita Bw. Hashim Rungwe aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, ulifanyika Desemba 17 mwaka huu, katika kikao cha NEC Taifa cha NCCR-Mageuzi, jijini Dar es Salaam.
Mwandishi Queen Lema, kutoka Arusha anaripoti kuwa, viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na wafuasi wao 19, jana wamesomewa mashtaka 13 yanayowakabili katika Mahakamaya Hakimu Mkazi Arusha na kukana yote ambapo leo, itaanza kusikilizwa.
Watuhumiwa wawili katika kesi hiyo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willbroad Slaa na mchumba wake Bi. Josephine Mushumbusi, kutokuwepo mahakamani hapo.
Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Bw. Charles Magesa, aliwataka washtakiwa waliofika mahakamani jana, kuhudhuria mahakamani leo bila kukosa.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka 13 likiwemo la kukiuka amri mbalimbali za mamlaka hivyo kusababisha vurugu zilizotokea Januari 5 mwaka 2011.
Wakisomewa mashtaka hayo na Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo, Bw. Edwin Kakolaki, mbele ya hakimu Bw. Magesa, alidaiwa kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo Januari 5,2011.
Bw. Kakolaki alidai kuwa, viongozi wa chama hicho na wafuasi wao, walifanya fujo kwa kuitisha maandamono na kusababisha kuvunjika kwa amani katika jiji hilo.
“Mheshimiwa Hakimu, hawa washtakiwa walikiuka sheria na matamko ya Serikali, walifanya mkusanyiko bila kuwa na kibali na kuwashawishi wananchi kuandamana katika maeneo mbalimbali ya jiji hili,” alidai Bw. Kalokola.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washitakiwa 17 walikana kuhusika nayo ambapo Hakimu Magesa, aliahirisha kesi hiyo na kuipanga leo.
Baadhi ya washtakiwa katika kesi hiyo ambao ni viongozi wa CHADEMA ni Mwenyekiti wa Taifa, Bw. Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dkt. Slaa, Mbunge wa Rombo, Bw. Joseph Selasini, Mbunge wa Moshi Mjini, Bw. Philimon Ndesamburo na Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema.
No comments:
Post a Comment