Na Suleiman Abeid, Shinyanga
MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mkoa wa Shinyanga, Bw.Steven Masele, amekiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanza kuwashughulikia kwa kuwavua magamba watendaji wote wa Serikali ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu na kusababisha chama kupoteza haiba kwa wananchi.
Bw.Masele alitoa ombi hilo juzi wakati wa maadhimisho ya chama hicho baada ya kutimiza miaka 35, zilizofanyika kimkoa Manispaa ya Shinyanga.
Alisema, badala ya viongozi wa CCM kujivua gamba ni vizuri chama chenyewe kingeanza kwa kuwavua magamba watendaji wa Serikali.
Alisema, pamoja na falsafa ya kujivua gamba kwa viongozi wa CCM iliyobuniwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, lakini ni vizuri sasa CCM ikawashughulikia watendaji wasio waadilifu ndani ya Serikali ambao vitendo vyao vinasababisha wananchi wakichukie chama tawala.
Bw.Masele alisema, Watanzania wengi wana imani na Chama cha Mapinduzi, ingawa wameanza kupoteza imani hiyo kutokana na jinsi ambavyo watendaji wake ndani ya Serikali wanavyoshindwa kuwatatulia kero mbalimbali zinazowakabili.
Alisema, iwapo CCM itashindwa kuwavua magamba watendaji hao ni wazi itakuwa na wakati mgumu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutokana na wananchi kukichukia zaidi.
Bw. Masele alisema, siku za hivi karibuni kumekuwepo malalamiko mengi dhidi ya watendaji wa serikali kuanzia makatibu wakuu wa wizara, wakurugenzi, taasisi za umma hadi ngazi ya mikoa na wilaya.
Alisema, baadhi ya watendaji wa Serikali wamekuwa wakitumia lugha chafu pale wanapowahudumia wananchi na mara nyingi hutanguliza mbele suala la kuomba kitu kidogo (rushwa) na hivyo kusababisha wananchi hao kukichukia chama tawala kwa vile kimeshindwa kuisimamia vyema serikali yake.
“Ndugu zangu ninawahakikishia kuwa hakuna mtu anayechukia CCM isipokuwa inabidi wafanye hivyo kutokana na matendo machafu yanayofanywa na baadhi ya watendaji,” alisema Bw. Masele.
Alisema, wapo watendaji wa Serikali ambao kwa makusudi wamekuwa wakihujumu miradi ya maendeleo inayopelekwa katika maeneo yao.
Alisema, baadhi ya makatibu wakuu wa wizara wamekuwa wakiingia mikataba mibovu ambayo madhara yake huwaelemea zaidi wananchi kutokana na kulazimika kulipa kodi zaidi ili kulipa gharama mbalimbali zinazotokana kusainiwa kwa mikataba mibovu.
No comments:
Post a Comment