06 February 2012

Mataifa ya kimagharibi yalivyoamsha chuki na somalia,Ethopia

MAKALA ya wiki iliyopita tuliona jinsi mataifa makubwa, hususan Marekani na Urusi,
yalivyochangia kuzuka hisia za chuki kati ya Somalia na Ethiopia.

Katika sehemu hii tutaona matokeo ya uchochezi huo.

Wakati Urusi na Marekani kila moja ikiijimarisha katika eneo hilo, nchi ya Ethiopia ilikumbwa na baa la njaa mwaka 1972 na 1973, ambapo ilikadiriwa kuwa katika kipindi kifupi cha miaka hiyo miwili, watu milioni 2 walikufa kwa njaa na maradhi, ikiwemo kipindupindu.

Hudaiwa kuwa kiongozi wa nchi hiyo, Mfalme Haile Selassie, ambaye alikuwa ni miongoni mwa watu mashuhuri duniani, ama kwa kuhofia umaarufu wake kutiwa doa hakutaka kufichua janga hilo la njaa kwa jumuiya ya kimataifa ili asaidiwe, au alifichwa na maofisa wake kile kilichokuwa kikitokea nchini humo, hususan mbali na mji mkuu, au yeye mwenyewe kutokana na umangimeza hakuwa akijishughulisha kufuatilia matatizo ya watu wake.

Kumbukumbu za kihistoria huaeleza kwamba Mfalme huyo, ambaye kabla ya kupewa jina la
Haile Selassie alijulikana kwa jina lake la asili la Ras Tafari Makonnen, alikuwa
ameitawala nchi hiyo kuanzia mwaka 1930.

Inasemekana kwamba, alikuwa ni mfalme wa 225 katika mtiririko wa ukoo wa Mfalme Sulemani wa Israel.

Janga hilo la njaa liliibua mfululizo wa migomo na maandamano ya umma nchini humo
kuitaka serikali Mfalme iingilie kati na kutatua matatizo ya wananchi wake.

Mfalme ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU)
ulioanzishwa mwaka 1963, hatimaye ghasia hizo zilisababishwa kuondolewa madarakani
Septemba 12, 1974. Alifariki akiwa kizuizini mwaka 1975 na kuzikwa kimyakimya.

Kuondolewa kwa Mfalme kulizua balaa kubwa nchini humo, ambapo wajumbe wa Baraza la
Muda la Utawala wa Kijeshi (EPMAC) likijumuisha askari 110 kutoka vikosi
mchanganyiko vya Majeshi ya Ulinzi, Polisi na Magereza, walianza kubaguana na kugombea uongozi na hivyo kuuana hovyo, hali ambayo iliiweka nchi hiyo katika janga la umwagaji damu, tofauti na lile la njaa.

Ikumbukwe kuwa tatizo la njaa bado lilikuwepo, serikali ya Mfalme ilikuwa
imeondolewa na sasa waliotarajiwa kuongoza nchi walikuwa katika hali tata na tete
ya kugombea madaraka katIka Mji Mkuu Addis Ababa.

Hapo awali, nilidokeza kwamba Mfalme alikuwa rafiki namba moja wa Marekani Barani
Afrika, na sasa akiwa ameondolewa kwa nguvu, tunaweza kusema nchi hiyo ilisuswa na taifa hilo kubwa la Magharibi, mwanya ambao ulitumiwa na Urusi ambayo pia ilikuwa
imejiimarisha kule Somalia.

Warusi walifikia makubaliano na baadhi ya wajumbe wa Baraza walioonekana kuwa na
msimamo mkali na kuwaahidi kuwasaidia kurejesha utulivu nchini mwao.

Hali hiyo ilisababisha mgawanyiko katika baraza, ambapo kundi hilo lenye msimamo
mkali likiongozwa na Kanali Mengistu Haile Mariam, lilipendelea msaada wa Urusi,
ambapo kundi lenye msimamo wa wastani lilitaka Ufalme uendelee kwa kumuweka mrithi
mwingine.

Kundi hilo lilikuwa la Mwenyekiti wa Baraza, Jenerali Amaan Andom ambaye alikuwa
kamanda maarufu aliyesomea nchini Uingereza.

Septemba 23, 1974, katika kikao kimojawapo cha Baraza, Mwenyekiti Andom alishinikizwa na kundi la akina Mengistu kuidhinisha kukamatwa na kuadhibiwa watu "wote", wakiwemo Mawaziri Wakuu wa zamani wa Serikali ya Mfalme, maofisa wa ngazi ya
juu waliokuwa wakituhumiwa kwa mambo mbalimbali, pamoja na baadhi ya wafanyabiashara maarufu.

Vyanzo vya kuaminika vinaeleza kuwa katika mojawapo ya mikutano ya asubuhi ya baraza
tawala, mwenyekiti huyo aliwataka wajumbe kumpa nafasi (kama mwenyekiti) ili aweze
kutathmini mapendekezo yote na kuamua mambo kulingana na alivyokuwa akiona inafaa.

Inaelezwa kuwa, majibu hayo ya Mwenyekiti Andom yalisababisha pande mbili hizo
kushindwa kuelewana, hali ambayo ilimfanya mwenyekiti na msafara wake kuondoka
mkutanoni na kwenda ofisini kwake na baadaye kwenda nyumbani kwake.

Huku nyuma mkutano uliahirishwa, lakini pia haikuishia hapo, kwani kundi la akina
Mengistu lilituma kikosi cha askari kwenda kumkamata Jenerali Amaan Andom.

Inaelezwa kuwa kule nyumabani kwa mwenyekiti huyo, yalizuka mapambani kati ya walinzi wake na waliotumwa kumkamata, ambapo katika kuzima upinzani huo nyumba yake ilipigwa kwa kombora na yeye kufariki.

Brigedia-Jenerali Tafari Benti aliteuliwa na Baraza kuongoza serikali hiyo ya mpito,
lakini kinyang'anyiro cha madaraka nchini humo kiliendelea kati ya Mengistu na kundi
lake, dhidi ya viongozi wenzake ambao hawakutaka mabadiliko ya haraka kuelekea
kwenye siasa za Kikomnisti.

Februari 3, 1977 pia wakati wa kikao cha baraza ambacho kilikuwa kikiongozwa
na mwenyekiti mpya, Jenerali Benti, yalizuka mabishano kati ya pande mbili hizo
kuhusu ajenda fulani, ambapo ghafla chumba cha mkutano huo kilivamiwa na kikundi cha askari ambao ni kama walitumwa.

Inadaiwa kuwa risasi zilirindima na kumwagwa kama mvua katika ukumbi wa mkutanoni ambapo, katika tafrani hiyo kubwa, jumla ya wajumbe 58 wa Baraza la Serikali ya Mpito, akiwemo Mwenyekiti Benti, waliuawa, huku Mengistu na baadhi ya wenzake wakinusurika.

Baadaye Mengistu aliteuliwa kuwa kiongozi mpya wa Ethiopia, na huo ukawa mwanzo wa
kutangazwa kampeni ya "Red Terror" (ukatili mwekundu), ambao mantiki yake ilikuwa
kuwatisha wapinzani wa serikali yake kwamba kama wangeendelea kuupinga utawala huo
mpya, wangekutana na ukatili wa kumwaga damu.

Licha ya Serikali ya Kanali Mengistu kufunga rasmi kambi za Marekani nchini humo, pia aliipa serikali yake jina la "Marxist-Leninist" (mfuasi wa Marx na Lenin), ambayo ni majina ya wanaharakati maarufu wa itikadi ya Kikomnisti duniani, ambayo misingi yake ni siasa ya ujamaa na kujitegemea.

Karl Marx (1818-1883) alikuwa ni wa Ujerumani, na hakuwahi kuwa kiongozi wa nchi,
ambapo Vladimir Lenin (1870-1924) alikuwa rais wa taifa kubwa la Muungano wa Nchi za
Urusi, ambao ulisambaratika mwaka 1991.

Hivyo, uamuzi wa viongozi wapya wa Ethiopia kufuata misingi ya siasa hiyo, ni hatua
iliyowafurahisha mno Warusi na washirika wao, na hasa kwa kuzingatia kuwa 'rafiki'
mpya alipokonywa kutoka mikononi mwa hasimu wao mkuu, yaani Marekani.

Kwa maneno mengine ni kwamba, kambi ya nchi za Mashariki, ikiongozwa na Urusi, iliona
kama ilikuwa imeikomoa kambi ya Magharibi iliyoongozwa na Marekani.

Sasa hebu turejee kuona wakati huo nini kilikuwa kikiendelea kule nchini Somalia.

Ni kwamba urafiki mpya kati ya Urusi na Ethiopia ulimaanisha kuwa sasa taifa hilo
lilikuwa na marafiki wawili (Ethiopia na Somalia) wasioelewana katika Pembe ya
Afrika.

Hata hivyo, ili kuendeleza urafiki huo, Warusi waliona vyema kuzipatanisha
Somalia na Ethiopia, lakini ilishindikana baada ya Somalia kukataa, na kutaka
irejeshewe Jimbo lake la Ogaden.

Msimamo huo wa Somalia uliifanya Urusi iamue kulekeza uhusiano wake wa hali na mali
kwa Ethiopia, ambapo Somalia nayo iliamua kuanzisha uhusiano na Marekani na hivyo
kupokea misaada mbalimbali.

Hapo ukatimia ule usemi maarufu kwamba "mpe msaada adui ya adui yako ili uweze kumtumia dhidi ya adui yako".

Misaada hiyo iliiwezesha Somalia kuwa na jeshi kubwa kuliko yote katika Afrika,
ambapo idadi ya askari na wanagambo ilitajwa kufikia kati ya 85,000 mpaka 100,000.

Jambo lingine la kukukmbuka ni kwamba Mfalme Selassie, ambaye aliitawala Ethiopia
kwa takribani miaka 44 kuanzia mwaka 1930 mpaka 1974, alisimamia kwa kiwango cha juu
suala la elimu kwa watu wake, ambapo wengi wa wasomi wa nchi hiyo walisomea katika
nchi za Uingereza, Marekani, na Ufaransa.

Hata Shirika la Ndege la nchi hiyo ambalo kwa wakati huu lina vituo 62 duniani, na ndio kubwa kuliko yote Barani Afrika, lilianzishwa mwaka 1945 kwa msaada
wa Marekani.

Msaada huo ulikuwa ni kuanzia fedha na watunzaji wake, marubani, wahandisi wa ndege,
na Meneja Mkuu, ambao wote walikuwa Wamarekani, na waliendesha shirika hilo kwa
miongo miwili na nusu mpaka mwaka 1971 shirika hilo lilipokabidhiwa kwa raia wa
Ethiopia.

Hii inanikumbusha usemi kwamba "unapotaka kufanya kazi yenye maslahi kwa taifa lako,
ifanya kwa kiwango cha juu", usibabaishe tu ilmradi ionekane kazi imefanyika.

Mfalme Selassie alipowaomba wageni hao wamsaidie kuanzisha shirika la ndege,
inadaiwa aliwaambia alikuwa akihitaji shirika la ndege lenye ubora na hadhi ya
kiwango cha Ufalme.

Ni hakika kwamba, wageni hao waliifanya kazi hiyo kwa viwango bora, na ndio maana
mpaka wakati huu ubora wa shirika hilo unaweza kuonekana popote duniani.

Hii inaonesha ni kwa kiwango gani nchi za Magharibi zilivyokasirika kuona Mfalme
huyo ameangushwa na wafuasi wa siasa za Kikomnisti.

Swali la kujiuliza ni kuwa kama Somalia, chini ya utawala wa Rais Siad Barre, ndio
ilikuwa na jeshi kubwa kuliko yote Barani Afrika, je, baada ya uongozi wake
kuanguka, askari wote hao na zana zao walikwenda wapi?

Ni kwamba wapiganaji hao waliingia mitaani, mijini na vijijini, ambapo matokeo yake
ni mkanganyika na vurugu ambavyo tunavishuhudiwa leo nchini humo.

Mnamo Julai 13, 1977, majeshi ya Somalia yaliivamia Ethiopioa kwa lengo la kutaka
kumega Jimbo la Ogaden na kulifanya kuwa sehemu ya ardhi yake.

Juhudi za Ethiopia kujaribu kujihami hazikufua dafu mbele ya Wasomali, na hivyo
kulazimika kuliachia Jimbo hilo kwa asilimia mia moja.

Majeshi ya Somalia yaliweza kuukamata mji maarufu wa Jijiga, ambao upo Mashariki mwa
mji mkuu Addis Abba, takribani kilometa 60 kutoka mpaka wa nchi hizo.

Wasomali walizidi kusonga mbele kwa kasi kuelekea Magharibi ndani ya ardhi ya jirani
yao, na kuanza kuupumlia mji wa pili kwa ukubwa upande wa Ethiopia wa Dira Dawa.

Kumbe sasa katika mazingira ya hatari namna hiyo, nchi inafanya nini kujinusuru kama
si kuomba msaada wa kimataifa?

Ni hakika kwamba ndivyo ilitokea kwa Ethiopia pale ilipoiomba msaada serikali ya
Urusi, ambayo iliitikia mara moja.

Urusi ilituma washauri wa kivita 1,500 na vifaa vyao, pamoja na ndege za kivita,
Cuba ilituma askari 18,000, wakiwemo marubani ambao baadhi yao walisomea Urusi, na
Yemeni ilituma wapiganaji 2,000.

Mataifa ya Mkataba wa kujihami wa Nchi za Ulaya Mashariki (Warsaw Pact), zilitoa
mchango wa fedha, vyakula, na mahitaji muhimu ya vifaa.Hiyo yote ilikuwa kumkabili
Mmarekani kwa uzito kule Somalia.

Mpaka kukamilika mandalizi yote hayo, majeshi ya Somalia tayari yalikwishafika
kwenye viunga vya miji mikubwa ya Harar na Dira Dawa, bila kutaja miji kibao hapo
katikati ambayo ilichukuliwa bila upinzani mkubwa.

Kuwasili kwa msaada huo mkubwa wa Kikomnisti kwa upande wa Ethiopia, kuliashiria
kuzuka vita ya uso kwa uso kati ya mataifa mawili huru, na ambayo mpaka sasa ndo
inahesabika kuwa kubwa kuliko zote katika Afrika.

Historia inayataja mapambano yaliyozuka kama "a vicious war" (vita kali).

Vita ilipiganwa ardhini na angani, huku ndege za kivita na vifaru kwa upande wa
Ethiopia vikiendeshwa na Wacuba wenyewe ili kumtimua mvamizi kwa ghadhabu ya aina
yake.

Hatimaye Majeshi ya Somalia yalizidiwa kete na kusukumwa mpaka ndani ya mipaka yao.

Hatimaye, wajumbe wa pande mbili hizo walikaa meza moja na kufikia muafaka wa kuacha
vita ilipotimu Machi 15, 1978.

Takwimu za vita hiyo zinazonesha kuwa mgogoro huo ulisababisha hasara na gharama
kubwa kwa pande zote, ambapo jumla ya wapiganaji walikuwa 106,000, miongoni mwao ni
Wasomali 49,000, Waethiopia 37,000, Wacuba 18,000, Warusi 1,500, na Wayemeni 2,000.

Jumla ya wapiganaji waliopoteza maisha ni 12,586, wakiwemo Wacuba 400 na Warusi 33.

Majeruhi wote ni 12,972, mateka pamoja na wanotajwa kuwa walipotea 4,175.

Hasara ya vifaa ilikuwa ndege za kivita 51, vifaru 211, magari ya kivita 138, na ya
kawaida 1,489.Kulikuwa pia na hasara za hapa na pale kwa raia kama ilivyo kawaida ya
vita.

Hivyo ndivyo Mataifa makubwa yalivyoamsha chuki kati ya nchi hizo mbili.

Mwandishi wa Makala haya anapatikana simu 0653005959.



No comments:

Post a Comment