06 February 2012

Elimu bora ndio msingi mkuu wa kupata wataala

TAIFA lolote duniani ili liweze kuendelea, linahitahi wataalam. Wataalam hao hawawezi kupatikana bila elimu.

Lakini pia, ili kupata wataalam bora ni lazima elimu bora itolewe kwa wanafunzi ambao ndio msingi mkuu wa kupata wataalam.

Elimu, inalenga zaidi kupata suluhu ya matatizo ambayo yanaikumbuka jamii mbalimbali, na ndio maana katika kutambua hilo, suala la ufundishaji unaozingatia kujenga uwezo umeanza kutumika hapa nchini.

Kwa kawaida, serikali pekee haiwezi kukamilisha kila kitu katika utendaji wa majukumu yake, na kutokana na ukweli huo ndio maana zikawepo sekta binafsi katika nyanja mbalimbali ili kusukuma maendeleo.

Katika Sekta ya Elimu, wadau wa elimu nao kwa nafasi yao wanatoa mchango kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa wanafunzi.

Na hivi karibuni, Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) kwa kushirikiana na Oxfarm na WaterAid ulifanya Kongamano la Uzoefu wa Utoaji Elimu Unaomlenga Mwanafunzi (COP), likiwajumuisha wadau wa elimu kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Katika kongamano hilo, mada mbalimbali zilijadiliwa, ikiwemo namna ya kuboresha elimu, kuanzia katika sekta ya ualimu hadi shuleni kwa wanafunzi, nia ikiwa ni kuhakikisha elimu bora inapatikana.

Lakini si elimu bora tu, bali hata mazingira ya kusomea na kufundishia nayo yanakuwa rafiki kwa wanafunzi na walimu.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na kuboresha upimaji wa mara kwa mara baada ya kufundisha kwa ajili ya maendeleo ya ujuzi.

Akielezea kwa undani hilo, Bi. Nancy Ng'winula anasema, ni vyema upimaji uanze kufanyika kabla ya kuanza kufundisha mada ili kujua mwanafunzi anafahamu nini juu ya kile anachoenda kujifunza.

Lakini pia, anafafanua kuwa kila baada ya somo, mwalimu atatakiwa kuhitimisha kipindi kwa kuwapa maswali ama kazi ya kufanya kwa kusudio la kuwapima kile walichojifunza na kufikiwa malengo mahsusi.

Japo zipo changamoto katika suala zima la upimaji, ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi vya kutosha, wingi wa wanafunzi na uchache wa walimu, lakini Bi. Ng'winula anashauri kuwa, ni vyema mwalimu akajiwekea utaratibu wa aina yoyote utakaosaidia upimaji wa mwanafunzi ili kuinua kiwango cha taaluma shuleni.

Bi. Joyce Andrew ambaye ni Mkaguzi wa Shule Manispaa ya Shinyanga anafafanua kuhusu kuimarisha upimaji ili kukuza ujuzi na kuongeza kuwa, ufundishaji unaozingatia ujuzi unatakiwa kumfanya mwanafunzi kuwa mbunifu katika tendo la kujifunza na kuyatumia yale aliyojifunza.

Anasema kuwa, mtazamo huo unamfanya mwanafunzi aweze kujenga maana ya kile alichojifunza na hivyo kufanya tendo la ufundishaji na ujifunzaji kuwa rahisi zaidi na lenye kumvutia mwanafunzi.

"Hata hivyo ili ujuzi na stadi ziweze kujengwa hatuna budi kuhakikisha kuwa, ufundishaji unakuwa sio ule ambao ni wa kumkaririsha mwanafunzi na badala yake uwe wenye kumjengea uwezo kiutendaji zaidi," anasema.

Anafafanua kuwa, suala la upimaji katika ufundishaji unahusu maudhui. Mwanafunzi anaelewa nini, anajifunza nini? Na kwa upande mwingine upimaji ni mchakato wa kuangalia namna gani mwanafunzi anajifunza.

"Hivyo upimaji unahusu uhusiano uliopo kati ya mwalimu na mwanafunzi katika mchakato wa kujifunza. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa sera na miongozo kadhaa inayosimamia upimaji katika elimu.

"Zipo njia nyingi, lakini ambazo zimekuwa zikitumika zaidi katika shule na nani ya darasa ni maswali na majibu, mazoezi wakati wa kufundisha na mwisho wa mada mitihani, majaribio ya wiki au mwezi pamoja na kitihani mikubwa ya kumaliza mihula, mwaka na shule," anasema.

Anaongeza kuwa, katika mbinu hizo za upimaji mitihani imepewa nafasi kubwa zaidi na hivyo hata mtazamo wa ufundishaji shuleni umefikia hatua ya kuathirika, kuyumba na kuwa mtazamo zaidi wa maandalizi ya kufaulu mitihani tu.

Katika kutatua hilo, Bi. Andrew anabainisha kuwa, lazima kuwe na mikakati ya kuhakikisha upimaji unalenga kupata picha ya maendeleo ya kukua kwa uelewa, kujifunza kwa kina na nyanja ya juu ya kufikiri, maarifa stadi na mwelekeo.

"Kwa kutumia zana za ufuatiliaji wa mwanafunzi mmoja mmoja kwa somo, mwalimu atatakiwa kutunza kumbukumbu juu ya yote aliyoyafanya na matokeo yake," anasema.

Na mada muhimu ilikuwa ni uboreshaji wa mafunzo ya ualimu, kwa kuwa inaeleweka wazi bila mwalimu hakuna ufundishaji wala elimu. Na Taaluma hii ni msingi mkubwa wa maendeleo kwa taifa lolote duniani.

Akiwasilisha mada hiyo Bi. Anitha Kihiyo anasema kuwa, taaluma ya ualimu ili iweze kuimarishwa inahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadau na wahisani wa elimu.

"Bila kuwa na msaada huo, Sekta ya Elimu itapoteza mwelekeo, changamoto zinazoikabili sekta hii zikiboreshwa na kufanyiwa kazi basi itasaidia kusonga mbele na hii itaifanya taaluma kuheshimiwa na watu wote," anasisitiza.

Mwanzoni alizibainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na kutokwepo kwa bodi inayotetea maslahi ya walimu, maadili ya kazi kwa walimu ambapo walimu walio wengi hawafuati misingi ya taaluma sambamba na uhaba wa zana za kazi kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia.

Changamoto nyingine anazitaja kuwa ni mishahara kwamba hailingani na taaluma nyingine, kukosekana kwa mafunzo ya walimu kazini ambapo huondoa ufanisi katika mbinu mpya za ufundishaji, maadili ya wanafunzi sambamba na uwezo wa walimu katika kuwasilisha mada.

Anasema kuwa, kutokana na changamoto nyingi zinaoikabili taaluma ya ualimu, zinatakiwa kuwekewa mikakati madhubuti ili kuifanya kuwa na hadhi na kutambulika kama taaluma nyingine.

Wakichangia katika kuboresha kila mdau wa elimu na maoni yake, wengine pia walishauri watoto wawezeshwe kupenda kujisomea, kwani hawapewi utamaduni huo tangu wakiwa shule ya msingi.

Na katika kuhakikisha hilo linafanikiwa ni pamoja na walimu kuandaa hadithi fupifupi sambamba na kuwaambia wanafunzi kufanya hivyo, lakini pia jamii ihamasishwe kutumia maktaba.

Sambamba na hilo, wengine walitupa shutuma kuwa walimu wanaojiendeleza kielimu hawataki kubaki katika tasnia hiyo na badala yake wanataka kwenda kwingine zaidi.

Akizungumzia mafunzo kazini, Mwalimu Ng'washi Kapaya kutoka Shinyanga analalamika kuwa, ana miaka 27 kazini na alikaa bila mafunzo kwa muda wote huo mpaka alipokuja kupata kwa ufadhili wa Shirika la Oxfam.

"Mwalimu anachotakiwa kufanya ni kumpa motisha mwanafunzi na ari ya kujifunza, kutengeneza mazingira ya urafiki na mwanafunzi pia inasaidia kufundisha vizuri.

Uhusiano huo si kazi rahisi kwa sababu si muda wote mwanafunzi anapenda kufanya mwalim anachotaka. Na ili uweze kufikia matakwa ya ufundishaji mbinu mpya zinatakiwa kila siku, na bila mafunzo kazini ya mara kwa mara huwezi kufanikisha hilo,"anasema.

Anaongeza kuwa mara nyingi mwanafunzi anapokosea, anatakiwa kuchunguzwa kwanza badala ya kumpa adhabu, na muda mwingine ni vizuri kujua historia ya mtoto.

"Adhabu haiwezi kuwa rafiki wa mwanafunzi, haimsaidii kujifunza. Ukimwadhibu anaweza kukaa darasani kimya akatengeneza sura kama anakuelewa kumbe ni kwa sababu ya kuogopa kuadhibiwa.

"Nia ni kumsaidia na kumpa ari ya kujifunza, muda mwingine tunataka kufanya kama tulivyofanyiwa na walimu wetu miaka ya nyuma, adhabu inawanyima watoto fursa ya kujifunza vyema," anafafanua.

Mkaguzi wa Shule Kanda ya Magharibi Bi. Sikudhani Ferdinand anasema, ili mwalimu aweze kufanya vizuri awe na mazingira mazuri yanayomuwezesha kufanya kazi.

"Mwalimu ili aweze kufanikiwa na kuwa mwalimu mzuri ni lazima pia we tayari kujifunza na awezeshwe.

"Ili kufanikisha mambo mengi katika elimu jamii isaidie sekta ya elimu, malengo yataweza kufikiwa, kila mmoja mwenye nafasi yake achangie kwa namna yoyote ile," anaongeza.

Abainisha kuwa Mwalimu Mkuu ni mkaguzi wa kwanza shuleni, kabla ya wakaguzi wa elimu kufika, hatua zichukuliwe kwa mwalimu legelege na hiyo itakomesha nidhamu mbovu kwa walimu wenyewe.

Pia washiriki wa kongamano hilo walishauri Kamati za shule kuwa na nguvu ili kufanikisha mambo ambayo ni muhimu kwa shule.

Kongamano hilo ni mfululizo wa makongamano yanayoandaliwa na TenMet kwa kuhakikisha kuwa elimu ya Tanzania inakidhi mahitaji na bora elimu kama inavyoonekana katika baadhi ya maeneo.

  

No comments:

Post a Comment