MALABO, Equatorial Guinea
TIMU ya Taifa ya Mali, imefanikiwa kushika nafasi ya tataui katika michuano ya fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kuilaza Ghana kwa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika usiku wa kuamkia jana mjini Malabo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kufanya vizuri tangu ilipofungwa katika mechi ya fainali mwaka 1972.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani (AP), alikuwa ni mchezaji Cheick Diabate ambaye aliipatia Mali mabao yote mawili ambayo yaliifanya Mali kulipiza kisasi cha mabao 2-0 ambayo ilifungwa katika hatua ya makundi.
Matokeo hayo yanaifanya Ghana kumaliza michuano hiyo kwa matokeo ambayo haikutarajia baada ya kuchapwa na Zambia bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali.
Mchezaji Diabate alifanya Mali iongoze baada ya kupatia bao dakika ya 23 na akaongeza jingine lililoihakikishia ushindi timu hiyo zikiwa zimebakia dakika 10 mpira umalizike.
Katika mchezo huo ambao ulifanyika kwenye Uwanja wa Nuevo Estadio de Malabo, Ghana ilijaribu kila hali ili kuhakikisha inaondoka na ushindi lakini bao lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake Sulley Muntari lilikataliwa kutokana na kuwa alikuwa ameotea kabla ya beki Isaac Vorsah, kutolewa nje ya uwanja dakika ya 64 baada ya kumfanyia madhambi Bakaye Traore.
Vikosi kamili vya timu hizo vilikuwa kama ifuatavyo,Ghana: Adam Kwarasey, John Pantsil, Isaac Vorsah, Jonathan Mensah, Samuel Inkoom (Prince Tagoe, 35), Lee Addy, Andre Ayew, Kwadwo Asamoah (Masahudu Alhassan, 68), Anthony Annan, Mohammed Abu (Sulley Muntari, 46), Jordan Ayew.
Mali: Oumar Sissoko, Cedric Kante, Adama Tamboura, Ousmane Coulibaly, Abdoulaye Maiga, Seydou Keita, Bakaye Traore, Samba Sow (Souleymane Keita, 85), Samba Diakite, Garra Dembele (Mustapha Yatabare, 86), Cheick Diabate.
No comments:
Post a Comment