06 February 2012

Jamii inaweza kuboresha elimu ya watoto wao

WATANZANIA wachache sana wanaoelewa kwamba ni  haki na wajibu kushiriki katika shughuli za elimu ili kuboresha elimu ya watoto wao.

Ushiriki huo unajumuisha kusimamia shughuli na maendeleo ya shule, kushiriki katika mikutano ya wazazi pamoja na mikutano mengine.

Vile vile kusimamia fedha za shule pamoja na maendeleo ya watoto wao ili kujenga uwezo wa kutoa maoni ya namna ya kuboresha elimu katika nchi hii.

Mara nyingi ushiriki wa wananchi umekuwa ukitazamwa na maofisa kama kuingilia masuala ambayo hayawahusu.

Ushiriki pekee ni uchangiaji wa fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za shule na si kushiriki kikamilifu katika mikutano kwa kutoa mawazo yao au kupaza sauti zao au kushiriki katika kupanga au kusimamia maendeleo ya shule.

Kwa hakika ni wananchi wachache sana ambao wanaelewa kwamba wana haki na wajibu wa kushiriki.

Asasi nyingi za kiraia nchini Tanzania zimeegemea katika kukuza demokrasia ili kuifanya demokrasia ikue.

Unahitaji wananchi wenye ukakamavu na uelewa ambao wanaelewa jinsi ya kudai maslahi yao, wenye kuchukua hatua kwa pamoja na wenye uwezo wa kuwawajibisha viongozi.

Serikali haina budi kuweka wazi na kwa lugha rahisi juu ya mchango wa kile ambacho jamii inapaswa kuchangia kwa ajili ya elimu wa watoto wao.

Ni muhimu iwekwe wazi iwapo wanaopaswa kuchangia ni wale tu wenye watoto shuleni au kila mwanajamii anapaswa kuchangia.

Uwezo wa kuchangia usiwe ndiyo kigezo cha mwanafunzi kunyimwa au kupewa fursa katika elimu.

Serikali ni muhimu ibuni mbinu itayowawezesha wazazi ambao hawajakamilisha michango yao kutoathiri maendeleo ya kielimu ya watoto wao.

Ni wazi kwamba kama hufahamu kinachotarajiwa kutoka kwao ni vigumu kuchukua hatua zinazofaa, serikali haina budi kuhakikisha kuwa wananchi wote wanatambua wanachotakiwa kufanya kuhusu maendeleo ya shule na uboreshaji wa elimu.

Ni muhimu kuwepo na kampeni  ya kitaifa inayoelezea uhusiano uliopo kati ya wananchi na kamati za shule, michango pamoja na faida za kufuatilia elimu ya mtoto, hali hiyo itasaidia kuondoa migogoro kati ya walimu na jamii.

Kampeni za mara kwa mara zinazoitaarifu jamii kuhusu faida ya elimu zitasaidia kupunguza athri za kimila zinazomnyima mtoto haki yake ya elimu.

 Iwapo hata baada ya miaka saba ya elimu ya msingi , watoto bado watakuwa hawajawa na uwezo wa kuandika majina yao, wazazi hawatakuwa tayari kuwaona watoto wao wakiingia mfumo ambao hauna faida zilizo dhahiri.

Kwa kutambua vipaumbele vya msimu katika jamii na kwa kuwa na ratiba inayoruhusu mabadiliko ili kuendana na hali ya maisha itawasaidia wazazi kuiona elimu kuwa ni kitu chenye faida.

Ushiriki hauna budi kuwa zaidi ya michango ya fedha, ni muhimu kwa wananchi kupewa taarifa za mara kwa mara kuhusu shughuli zinazofanyika shuleni pamoja na kile ambacho watoto wao wanajifunza shuleni bila kusahau jinsi tathmini inavyofanyika.

Wananchi wasiishie kupokea ripoti pekee bali wapewe fursa ya kujadili pamoja na kuuliza maswali..

Changamoto hiyo isiishie kwa wanafunzi pekee bali ihusishe pia tathmini kuhusu mapato na matumizi ya shule pamoja na sera na mipango ya mandeleo ya elimu katika ngazi za wilaya hadi vijiji, uwepo wa ubadilishanaji wa maarifa na uelewa ulio wazi utaongeza ushiriki wa jamii.

Serikali pamoja na Asasi za Kiraia ni lazima ziwajibike katika kuwajengea wananchi ushiriki wenye tija ili waweze kushiriki kikamirifu katika jamii.

Zana zinazoweza kuwasaidiwa wananchi kuwa na ushiriki wenye tija zinazojumuisha maarifa juu ya haki na wajibu wao pamoja na maarifa ya jinsi ya kudai haki zao kwa maneno meangine kuwajengea wananchi uwezo wa kuchukua hatua.


No comments:

Post a Comment