06 February 2012

Wako wapi wenye wito?

KAZI ni wito… kazi ni wito.. ulikuwa ni wimbo wa watumishi wa serakali, wanainchi na viongozi wa Danganyika hii miaka hiyo ambayo angalau kulikuwa na mwangaza wa maisha bora.

Enzi za maduka ya RTC, enzi ya maduka ya Ushirika enzi hizo kila mkoa ukiwa na Kampuni zake za usafiri, Mwanza wakiita KAUMWA, Tanga wakiita KAUTA, Dsm wakiita UDA, Dodoma ikaitwa KAUDO nakadharika wa kadharika.

Eni hizo ambapo tulikuwa na viwanda vyetu vya mazulia huko Kilosa, Kiwanda cha kusindika nyama tukakiita Tanganyika Peakers, kiwanda cha maturubai ‘canvas’ huko Morogoro, tuliendelea hadi tukawa na kiwanda cha kukata
madini yetu pale Iringa wenyewe tukakita Tancut.

Ilifikia mahali, ikawa ni fahari kwa mtumishi kuimba wimbo huo, utasikia… “Mimi mwalimu bwana, hii ni kazi ya wito”..mwingine atakwambia “ mimi dokta kweli bwana hii ni kazi ya wenye wito”…

Kila kazi ilikuwa ya wito, isipokuwa wizi, udokozi, ujambazi na ukahaba na kazi nyingine kariba ya hizo, kwa hiyo ili kuingia katika ajira ya serakali hapana shaka ilikuwa iwe lazima ‘umewiwa’!

Halafu ikawepo ile kitu iliyoitwa Neshino Sevisi yaani Jeshi la Kujenga Taifa, yaani JeiKeiTii na kule Zenji likaitwa Jeshi la Kujenga Uchumi, yaani JeiKeiYuu, maisha yakasonga mbele huku tukiambiwa kuwa majeshi haya yalikuwa mahsusi kwa ajili ya kumjenga mwanainchi maadili na uzalendo.

Leo hii naambiwa maadili ya Mdanganyika yameporomoka kwa kiasi kikubwa sana, wengi wanazungumzia kufutwa wanaosoma kwenda Neshino Sevisi kwa mujibu wa sharia, kwamba ndiko kumesababisha kuporomoka na kumong’onyoka kwa maadili.

Lakini ukweli kiasi gani unathibitisha nadharia hii ya kwamba kungalikuwepo Neshino Sevisi tusingekumbwa na baa la Richard Mond na Doa la Inzi, kwani hao wanaofanya hayo madudu hawakupita Neshono Sevis?

Nambieni enyi Wadanganywa kama kweli wale wezi wa Eleza Pesa Alikopeleka eikeiei KWEPA kama nao hawakupita hiyo Neshino Sevisi yenu, na hao walioingi mikataba kama ya akina Karl Peters wakanunua machuma machakavu mkaita ndege ya RaHis na rada pia hawakupita Neshino Sevisi?

Hawa wanaoingia mikataba ya madini ya ajabu ajabu nao hawakupita Neshino Sevis? Au mwawaonea hao wakusoma katika vyoo vikuu na wengine wanapoandamana kudai chao, ninyi mwanena ya kuwa hawana maadili kwakuwa hawakupita Neshino Sevis!

Kwa hiyo tunakubaliana kuwa hiki ni kizazi cha nyoka kisicho na maadili wala wito wa kazi, si mimi wala si wewe hakuna mwenye maadili wala wito, si wanafunzi wa vyuo wala sekondari, hakuna cha madokata kweli wala maticha!

Kama ndivyo basi ni kweli siku hizi Kazi ni kijiwe cha biashara, dhana na nadhari ya kutoa huduma haipo! Kwani mwataka kujifanya mmesahau wale wenye kuvaa nguo nyeupe walipogoma na kucheza sindimba na kiduku tena wakisindikizwa na matarumbeta wakiandamana kugoma kutoa huduma na raia kibao wakafa mawodini?

Ndiyo hadithi inayokuja sasa, fukuto la mgomo wa wavaa makoti meupe, hawa wakigoma watahanikiza na maticha wagome, nao watahanikiza kada nyingine zigome, ndivyo ilivyo kama madai yao yana msingi tuwaunge mkono kama hayana msingi tuwapuuze!

Sote twajua inchi hii inavyokwenda, mwisho wa siku tutapata maticha na machita (teachers and cheaters), mwisho wa siku tutapata wahandisi na waandishi, hapa kuna ‘waandishi wa habari na wahandisi wa habari mnaowaita makanjanja’ lakini kuna watu wa fani ya uhandisi ambapo matokeo yake tunawapata wahandishi wa majengo na fani nyingine badala ya wahandis!

Badala ya kufanya kazi za uhandisi wao wanafanya kazi za uandishi, kwani wavaa makoti meupe wote ni madoktari? Mbona wachinja nyama buchani nao wanavaa makoti meupe? Hata wahuduma wa mama lishe na wale wa hotelini nao wanvaa makoti meupe, naam wamenena ya kwamba mnyonge mnyongeni lakini chake
mpeni!

Nami namiulizeni leo, hivi kweli nani amebaki muadilifu na mwenye wito? Leo nani anafanya kazi ya wito? Tusiongopeane, wote tumekuwa ‘majizi’  na hakika watakaokuwepo wazima hadi siku ya mwisho wakati Mwenyezi atakapokuwa anayaanika madhambi ya kila mmoja hadharani kutakuwa na aibu sana maana
unayemdhani siye kumbe ndiye!

Hebu niambieni huo wito ni upi dunia hii ya leo enyi mnaoendelea kuhubiri injili hii tamu ya wito katika kazi? Ndiyo maana sishangai hata kiduchu kusikia leo askari anakuwa jambazi mchana kweupe, au mwajifanya hamna taarifa ya askari aliyekamata dawa za kulevya akazing’ng’ania kama kidhibiti kisha akaingia nazo mitini?

Mtahubiri sana habari za watumishi wa serakali kuwa na wito, kwani imeshawatoka kichwani mara hii ile ya juzijuzi askari kukamata mahindi kama kidhibiti kisha naye akaingia nayo mitini? Je  aliyekamata mapene ‘dolari’ za Marekani? Naambiwa naye alilala  nazo mbele!

Acha hivyo, kwani mara ngapi mnawafichia siri askari wanaotumia silaha na risasi walizokabidhiwa kwenda kufanyia ujambazi?  Hao wavaa makoti meupe ni mara ngapi yairabi wanaiba dawa na kuweka kwenye viduka vyao vya dawa na zahanati? Hawa wavaa mavazi meupe nao naambiwa baadhi yao  wana lugha chafu kama wamemeza kanda mpya za matusi!

Huu wito mnaohubiri ni upi? Hakuna mwenye wito dunia ya leo kama wapo wamebaki wawili kama alivyoimba hayati Marijan Rajab, kwamba katika watu mia binadamu amebakia mmoja!  Hao walimu mbona naambiwa kazi yao ni kutembea na wanafunzi? Kwani hili liko Praimare na Sekondare tuu? Mbona huko Vyoo Vikuu mnaita alama za Chu-P?

Namiambieni hata hao maprofu wenu nao wanahusudisha uroda wa ubwete na wa ghafla, ukienda shule za sasa unashindwa kujua mwanafunzi ni yupi na mwalimu ni yupi, wote  wanavaa mtepesho eikei mlegezo yaani ‘kata Kndu’.. na sasa wanaita vimodo!

Walimu wa kike nao wanavaa vivazi kana wameazima kwa wadogo zao na sasa vimewabana, shehena na matiti nusu nzima inaning’inia nje? Kwanini asiombwe uroda hata na wanafunzi wao, na kwakua ‘hapendwi mtu ila pochi’ mambo yanakwenda!

Ndipo utakapoamini ya kwamba kweli hapendwi mtu ila pochi kwa sasa na hakuna cha wito wala maadili mbele ya njuruku, hakuna nidhamu mbele ya mapene na mapene yenyewe ndiyo haya kila siku thamani ya shilingi inashuka kimtindo, tufanye nini, ufe njaa wakati mkononi unamidhibiti cha dola ya Mmarekani? Dhubutu, ni kulala mbele tu mtu wangu!

Hali mbya, hali za wanainji duni na ufukara wa hali ya juu, tusidanganyane kwa lolote, katika hali ya ufukara kama huu huku wachache wakineemeka kwa jasho la wengi hakuwezi kuwepo uadilifu wa kweli, hakuwezi kuwepo wito, hakuwezi kuwepo ari ya kazi badala yake ni migogoro na maandamano yasiyokwisha,
wadanganyika wanashuhudia ya kwamba sasa ni Bora maisha na Si Maisha Bora kwa Mdanganyika, kifuatacho aitivii ni nini kama si haya tunayoshuhudia leo?

Hata zingekuwepo hizo mnazoita Neshino Sevizi kumi elfu, kama Mdanganyika anaishi bora maisha na si masiha bora hakuwezi kuwa na amani, litazuka hili upande ule na kule litazuka lile, mwisho wa siku ndiyo mambo ya kuchezewa mdundiko na matarumbeta huku walala hoi wanakata roho ‘mahosibitalini’ kwa
kukosa huduma!

Namiulizeni enyi mnaohubiri wito katika kazi, nani amebaki na wito? Wito kwenye maisha ya kila siku afadhali ya jana? Maisha ya kuumangia nguru wa kubanikwa? Huwezi kuishi kwa kula dagaa wawili mchuzi debe! Huu si Udanganyika,  wako wapo wenye wito?



-Nambieni mimi Mlala Hoi AM-


No comments:

Post a Comment