03 February 2012

HUDUMA katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN) zimeendelea kuwa mbaya

Kutokana na idadi ya wagonjwa kupungua kutoka 100 hadi 25  kwa siku hali inayosababisha vitanda kuwa wazi wodini.



Gazeti hili lilitembelea Wodi ya Kibasila na Siwahaji  Mwaisela,na kujionea hali ilivyo huku wodi nyingine zikiwa na wagonjwa sita na vitanda vingine vikiwa vimetandikwa havina wagonjwa.

Hata hivyo  idadi ya watu wanaoingia katika hospitali hiyo zimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea nchi nzima, hali hiyo imesababisha  hospitali hiyo kuwa kimya tofautio na siku za nyuma.

Vile vile baadhi ya wagonjwa waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa huduma hazipo kabisa hasa kwa wagonjwa wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji .

"Hali ya huku wodini siyo nzuri kabisa kwani mimi nimekaa hapa wiki mbili natakiwa nifanyiwe upasuaji  lakini cha kushangaza juzi tulitayarishwa  kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji ,tulipofika katika vyumba vya upasuaji tuliambiwa turudi kwani madaktrai hawapo,"alisema Mmoja wa wagonjwa Upendo Msangi.

Alisema kuwa kitendo kile kinawaumiza sana kwani ingekuwa  ni Ndugu yake waziri au wabunge ungekuta wameshapelekwa India kwa ajili ya matibabu lakini kwa vile hakuna ndugu zao hapo ndo maana serikali inawaumiza.

Serikali inatakiwa kukaa nchini na kusikiliza kilio cha madaktari kwani wasipofanya hivyo watu wanaoumia ni wa kipato cha chini ambao hawawezi kumudu gharama katika hospitali  Binafsi.

Naye Meneja wa  kitengo cha dharura Dkt. Silanda Optatus alisema kuwa  bado hali siyo nzuri katika hospitali hiyo kwani kwa sasa  wagonjwa wanafika  wachache tofauti na kipindi cha nyuma.

Alisema kuwa  kitendo hicho kilikuwa kinapokea wagonjwa 80 hadi 100 kwa siku lakini kwa sasa wameshuka na kufikia  25, hali ambayo siyo nzuri kwa hospitali kubwa kama hii.

Pia Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi Bw.James Mbatia alisema  kuwa katika hospitali ya Amana na Muhimbili ambazo ametembelea hali ni mbaya sana kwani serikali inatakiwa kukaa meza moja na kutatua mgogoro huo .

Alisema kuwa Mgogoro huo ukiendelea unaweza hata  kuiondoa serikali iliyoko madarakani 2015 kwani siyo sikivu kwa wananchi wake.

"Mwaka 1992 ulitokea mgomo kama huo katika hospitali hiyo ya Taifa Muhimbili wakati serikali ikiongozwa na Rais Mstaafu Ali Hassani Mwinyi walitumia busara  na kukaa pamoja na madaktari na kumaliza mgogoro huo.

Hivyo serikali inatakiwa kutumia hekima na busara zilizotumika  kipindi cha nyuma  kukaa nao na kuzungumzia madai wanayoyataka ili wananchi waendelee kupata huduma kama kawaida.

Pia alisema kuwa serikali ikubali haina madaktari wa kutosha katika sekta mbali mbali, hivyo ni vyema wakatumia busara kukaa na madaktari kuzungumza na kufikia muafaka kwani maisha ya wananchi yanazidi kupotea.

Hata hivyo alisema kuwa Serikali ikumbuke kuwa  malengo ya Milenium waliojiwekea ya kupunguza  vifo vya akili mama na watoto  ifikapo mwaka wa 2015 itakuwa  kazi bure kwani madkatari ambao wangetibu wagonjwa ndo hao serikali inawawekea ngumu.




No comments:

Post a Comment