06 February 2012

Gratian Matovu afariki dunia

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limekipata pigo kutokana na kifo cha mwamuzi wa zamani wa kimataifa, Gratian Matovu kilichotokea juzi nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Licha ya kuwa mwamuzi, Matovu aliyezaliwa Novemba Mosi 1926 aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT), sasa TFF mwishoni mwa miaka ya 1990. Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa Matovu alifariki dunia juzi.

Alisema vilevile aliwahi kuwa mkufunzi wa waamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na pia kamishna wa shirikisho hilo.

Ofisa huyo alisema msiba uko nyumbani kwake, Mbezi Beach Makonde na shughuli za kumuaga marehemu zitafanyika hapo hapo kesho kuanzia saa 5 asubuhi.

Alisema kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Steven Matovu baadaye mwili utasafirishwa kwenda Karagwe mkoani Kagera kwa maziko ambayo yanatarajiwa kufanyika Februari 9 mwaka huu.

Wambura alisema msiba huo ni pigo kwa familia ya Matovu, TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa kwa Tanzania, hasa wakati akiwa mwamuzi na mkufunzi wa waamuzi.

“TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Matovu, Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake,” alisema Wambura.

Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina


No comments:

Post a Comment