03 February 2012

Fomu za wagombea DRFA kuanza kutoka leo

Na Zahoro Mlanzi

MCHAKATO wa Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), unaanza leo kwa kuanza kutolewa fomu ambapo fomu za kuwania nafasi tano za juu ni sh. 500,000 kila moja.



Nafasi hizo ni Mwenyekiti na Makamu wake, Katibu Mkuu na Msaidizi wake na Mhazini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa mkoa huo, Muhdin Ndolanga alisema mchakato wa kupata viongozi wapya wa chama hicho, unatarajiwa kuanza leo kwa kutolewa fomu katika ofisi za chama hicho.

"Mchakato huo utaanza kesho (leo) mpaka Machi 18, mwaka huu ambapo ndiyo siku utakaofanyika uchaguzi wenyewe, hivyo tunawaomba wadau wa soka wenye sifa mbalimbali kujitokeza kuchukua fomu," alisema Ndolanga.

Alisema kwa nafasi za juu kama uenyekiti, ukatibu mpaka uhazini ni sh. 500,000 lakini Uwakilishi wa klabu pamoja na Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni sh. 300,000 na Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni sh. 200,000.

Ndolanga alisema fomu zitatolewa mpaka Februari 13 mwaka huu, ambapo kamati yake itafanya uchambuzi wa wagombea na siku mbili baadaye watawaita kwa ajili ya kuwafanyia usaili.

Alisema baada ya kazi hiyo Februari 16 na 17 zitakuwa ni siku maalumu kwa ajili ya pingamizi, ambapo kama kutakuwa na wagombea wanaoonekana machoni kwa wadau hawana sifa ndiyo kipindi chake cha kuweka pingamizi.

"Mchakato huo lazima uwe mrefu kwani kupata viongozi bora lazima umakini uwepo ambapo, baada ya pingamizi hizo kupitiwa Februari 22 watatoa orodha ya mwisho kwa watakaogombea," alisema Ndolanga.

Aliongeza baada ya shughuli hiyo kukamilika ndipo kampeni zitaanza kwa wagombea kujinadi na baadaye kufanya uchaguzi katika ukumbi utakaotangazwa baadaye.






No comments:

Post a Comment