03 February 2012

Bongo Movies, Kadansi FC kuchuana J'pili

Na Mwali Ibrahim

KAMPUNI ya Compact Media, imeandaa mchezo wa hisani kwa ajili ya kuchangia waathirika wa mafuriko yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana, Dar es Salaam.

Mchezo huo utazikutanisha timu za soka zinayoundwa na wanamuziki kutoka katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi nchini 'Kadansi FC' na timu ya wasanii mbalimbali wa filamu na uchekeshaji 'Bongo Movies'.

Mchezo huo unatarajiwa kufanyika Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo kutakuwa na burudani kutoka kwa wanamuziki hao, ambao wataunda bendi moja na kuimba kwa pamoja huku.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Compact Media Eliya Mjatta, alisema viingilio katika mechi hiyo ambayo wameamua kuipa jina la 'Tuwasaidie waathirika wa mafuriko Dar es Salaam' kitakuwa sh. 2,000 kwa majukwaa yote kasoro VIP, ambako kitakuwa sh. 30,000.

"Tumeamua kuweka viingilio hivyo ili kuwapa nafasi watu wengi kuhudhuria mechi hiyo, ili kufanikisha kupatikana kiasi cha fedha kwa ajili ya kusaidia jamii zilizokumbwa na mafuriko," alisema.

Alisema wasanii hao wapo tayari kushiriki mchezo huo kutokana na kuguswa na matatizo hayo, huku wakizingatia wananchi hao ndiyo miongoni mwa wateja wa kazi zao hivyo ni nafasi yao kuwaonesha upendo.

Mjatta alisema kila timu ina mlezi wake ambapo Bongo Movies FC ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki na Kadansi FC ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Suleima Kova.

Aliongeza kuwa zawadi za washindi katika mchezo huo ni mfano wa kombe halisi la Dunia.

Alisema leo wanatarajia kwenda katika maeneo wanayoishi waathirika hao waliopewa na serikali, Mabwe Pande kwa ajili ya kuangalia matatizo yao ya msingi ili fedha zitakazopatikana katika mchezo huo zitumike kwenye kutatua matatizo hayo.

Naye Kocha wa timu ya Bongo Movies, Niki Mchoma 'Chiki' alisema timu yake ipo tayari kwa ajili ya kuikabili Kadansi FC, kwani wamejipanga pia kutoa burudani ya kutosha kwa mashabiki na hata kuchukua ushindi.

"Waliopata matatizo ni mashabiki zetu na ni wateja wa kazi zetu, hivyo tumeguswa na tumejipanga kuhakikisha tunafanikisha kupatikana kwa fedha ili kuwasaidia," alisema Chiki.

Kwa upande wake kocha wa Kadansi FC, Muimbaji wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Muumini Mwinjuma alisema wao wamejipanga kuwafunga wapinzani wao na kuwataka wasiingize mamluki.

"Yupo Ally Choki ambaye ni kocha pia, Charles Gabriel 'Chaz baba', Traasis Masela, Christian Bella, Khalid Chuma 'Chokoraa', Kalala Hamza 'Kalala Junior' na wengine wengi hivyo burudani itakuwa ni ya uhakika na ushindi ni lazima," alisema.


No comments:

Post a Comment