08 February 2012

Dkt.Shein atoa somo kwa vyombo vya sheria Z'bar


 Mwandishi Maalumu, Ikulu Zanzibar                                                                         
RAIS wa Zanzizbar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amesema katika kuhakikisha sheria zinafuatwa na haki inatendeka, ni lazima wahusika wote wakiwa ni watendaji katika vyombo vya sheria, mahakama, taasisi za kodi na taasisi za kutoa huduma mbalimbali kuzingatia ukweli na uadilifu.
Dkt. Shein aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, yaliyofanyika katika viwanja vya Victoria Garden mjini Zanzibar ambapo Rais Shein aliwapongeza waandaaji wa maadhimisho hayo kwa mara ya kwanza visiwani humo.

Alisema, kwa upande wa mawakili na mahakimu anaelewa kwamba kabla ya kuanza kazi wanakula kiapo ambacho kinatamka wazi wazi kuwa watafanya haki bila ya woga, chuki au upendeleo.

"Hivyo suala hilo ni la maadili ambalo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inalitilia mkazo mkubwa kwa watendaji wote serikalini," alisema.

Dkt.Shein alitahadharishwa kwamba baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Utumishi wa Umma 2011 vitendo vya rushwa na vingine vinavyoenda kinyume na maadili havitavumiliwa tena.

Alitoa wito kwa watu wote kuwa macho na kuacha tabia ya kuachilia au kufumbia macho uvunjaji wa sheria na maadili kutokana na woga au kumuonea mtu aibu.

“Utekelezaji wa sheria unatoa haki kwa watu na unaleta amani na utulivu ndani ya jamii na unajenga imani za watu kwa vyombo vya sheria...utekelezaji wa sheria usioridhisha ndio hatimaye unaoleta madhara ndani ya jamii,”alisema Dkt. Shein.

Alisema, ni ukosefu wa utekelezaji wa sheria, pale ambapo watu wanavunja sheria kwa kujenga katika vyanzo vya maji, unapofanyika ukataji wa miti ovyo na uharibifu wa mazingira kwa jumla ambapo vyombo vya sheria vinavyohusika na watendaji wake wamekuwa hawatilii mkazo utekelezaji wa sheria zinazohusu mambo hayo.

Akitolea mfano Dkt. Shein alisema, kama inavyoelewekwa kwamba rushwa isipodhibitiwa inapelekea vyombo vya kutekeleza sheria kama vile mahakama, polisi, wakusanyaji mapato na wengineo kutotekeleza wajibu wao ipasavyo ambapo mambo hayo yakitendeka mwananchi anaweza kunyimwa haki ya kisheria.

Pamoja na hayo, Dkt.Shein alieleza kufarajika kwake kutokana na maadhimisho hayo ya siku ya sheria chini ya kauli mbiu ‘Piga Vita Rushwa katika Utoaji Haki’.

No comments:

Post a Comment