08 February 2012

Wabunge waibana serikali sakata la gesi asilia

*Washangazwa na majibu yake, wasisitiza umakini zaidi
Na Michael Sarungi
WABUNGE wameiweka Serikali kitimoto baada ya kutoridhishwa na majibu yake juu ya taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya bunge kuhusu matatizo yanayoikabili sekta ya gesi asilia nchini.
Mjadala huo uliibuka bungeni mjini Dodoma jana baada ya Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja, kuwasilisha taarifa yake ambapo Mbunge wa Mwibara, Bw. Alphaxard Kangi, aliikataa na kuishangaa Serikali kuikumbatia Kampuni ya Pan African Energy.

Bw. Kangi alisema, kampuni hiyo imeiibia Serikali fedha nyingi, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

“Hawa ni wazungu gani, tunawafahamu na bado tunaendelea kuwaangalia, hili suala linapaswa kuangaliwa vizuri, kwanini tuendelee kujadiliana nao,” alihoji Bw. Kangi.

Aliongeza kuwa, Serikali imetoa maelezo ambayo ameshindwa kuyaelewa na kusisitiza kuwa, Tanzania imechoka kugeuzwa shamba la bibi hivyo hakuna sababu kukumbatia kampuni hiyo.

“Kimsingi inashangaza sana, leo hii mwizi tumemkamata, lakini tunashindwa kuchukua hatua, hizi fedha zingepatikana, (mgomo wa madaktari), usingetokea kama ilivyo sasa,” alisema.

Mbunge wa Bumbuli, Bw. Januari Makamba, alisema kilichotolewa katika majibu ya Serikali ni ahadi si majibu ya matatizo.

Aliitaka Serikali kuwa makini inapoingia mikataba na baadhi ya kampuni za kigeni ambazo nyingi zinatanguliza maslahi binafsi bila kujali ya nchi husika.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bariadi Mashariki Bw. Jonh Cheyo, alihoji kwanini Serikali inashiriki kuua Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa kuunda kitu kinachoitwa Kamati ya Serikali ya Upatanishi ambayo Mwanasheria Mkuu ni mjumbe wake.

Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika,  alihoji umakini wa Serikali katika suala zima la kuwajibisha watumishi wake ambao wanakiuka maadili yao ya kazi.

Alitumia fursa hiyo kurejea maazimio ya bunge kuhusu Kampuni ya Richmond na utekelezaji wake kwa ujumla. Aliitaaka Serikali kuhakikisha inakuwa makini hasa inapoingia mikataba na kampuni za kigeni ili kulinda rasilimali za nchi.

Bw. Mnyika alihoji uhalali wa Wizara hiyo kushindwa kutoa ushirikiano wa dhati kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Madini (EWURA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) badala yake imekuwa ikitoa ushirikiano kwa kampuni ya kigeni ya Pan African Energy.

“Serikali kila mwaka inakuwa na mikakati mingi isiyoweza kutekelezeka badala ya kujibu  maswali magumu yanayoulizwa kila mara,” alisema Bw. Mnyika.

Mbunge wa Muhambwe, Bw. Felix Mkosamali, aliishauri Serikali kuwahurumia Watanzania waishio chini ya dola moja kwa siku.

4 comments:

  1. sawa ndugu zetu wabunge,lkn Ngereja alishashindwa kabisa ila boss wake naye kawa mgumu kumwajibisha

    ReplyDelete
  2. Serikali ya Kikwete haina nia ya kumaliza tatizo la umeme Tanzania. Inashangaza sana inatumia fedha nyingi kulipa haya makampuni wakati kama tungejibana fedha hizo zingeweza kuweka vyanzo vya kudumu vya umeme bila kulipa hayo makampuni. Hii ni serikali ya ajabu sana isiyotaka kusikia vilio vya wananchi na haina nia njema ya kliendeleza taifa hili

    ReplyDelete
  3. Hivi tumewahi kujiuliza sababu zilizomfanya Chief Magungo wa Msobero kusaini mkataba na Wajerumani wakati wanaingia Tanzania miaka ya 1800 na kujikuta nchi yake yote amewapa wajerumani na kisha wakamnyonga?

    Kwanza yeye aliamini ana akili kuliko watu wake wote! Pili alijua anasaini mkataba wa urafiki na watu wema kabisa , marafiki zake!

    Ukweli ni kwamba alikua mjinga sana na wajerumani walikua werevu sana. Kwanini hali hii inatokea hadi sasa viongozi wetu wanaposaini mikataba na wageni? Kwanini upande wetu unakua na wajinga wanatuwakilisha na wenzetu ni werevu siki zote? tatizo nini?

    ReplyDelete
  4. kuna mtumishi mmoja wa serikali alikamatwa kwa rushwa ya Tsh. 6000/= wilaya moja ya mkoa wa mwanza, ambapo mpaka mkuu wa wilaya alikuja kuhakikisha mtumishi huyo anakamatwa, tulisifu sana kwa juhudi na nguvu zilizotumika kumkamata mtumishi huyu, lakini nikabaki nashangaa mbona nguvu hizi huwa sizioni au kuzisikia katika mambo makubwa kama haya, yenye kuhusisha viwango vikubwa vya pesa, ambazo zinaweza kutatua matatizo makubwa yanayotukabiri watanzania.
    au, huyu mtumishi aliyekamatwa kwa nguvu nyingi nikutokana na kwamba rushwa yake alikula yeye peke yake hakumpatia DC, na hao viongozi wengine waliokuja kumkamata. am kweli mwenda tezi naomo mngojee ngamani.

    ReplyDelete