Na Rachel Balama
NCHI wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimekubaliana kuanzisha mpango mkakati wa amani na usalama kwa lengo la kupambana na ugaidi na uharamia katika Bahari ya India.
Pia EAC itabeba jukumu la utatuzi wa migogoro na kupambana na biashara ya dawa za kulevya, ili kudumisha usalama na amani kwa nchi wanachama.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Siasa, Ulinzi na Usalama wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Kagyabukama Kiliba, alipozungumza na waandishi wa habari.
Bw. Kiliba, aliyataja malengo mengine ya mkakati huo kuwa ni kuimairisha usalama katika ziwa Victoria, kuandaa mfumo wa kushughulikia migogoro katika kanda hiyo, kuimarisha mawasiliano na kuimarisha operesheni za pamoja.
Aliongeza kuwa ili kuimairisha ubadilishanaji wa taarifa za uhalifu, kubadilishana taarifa za hali ya usalama, kuimairisha mawasiliano, viongozi wa usalama kutembeleana, kupambana na wizi wa mifugo na kutekeleza mradi wa kudhibiti kusambaa kwa silaha ndogo haramu.
Alisema ili kutekeleza mpango huo kikamilifu, alisema nchi wanachama zimekamilisha majadiliano ya itifaki ya amani na usalama ambayo ni mtambuka.
Alisema moja wapo ya njia kuu za kuepuka migogoro na maafa ni kung'amua mapema viashiria kwa kuwa migogoro inaweza kuwa ya kijamii, kiuchumi, kisiasa lakini pia maafa kama njaa, ukame na mafuriko.
Alisema Jumuiya imekubaliana kuunda mfumo wa upashanaji habari kama njia ya kuepuka migogoro na maafa, uundwaji wa mfumo huu ni maandalizi ya utekelezaji wa itifaki ya amani na usalama.
Kuhusu rasimu ya mpango wa kusuluhisha migogoro kwa njia ya amani, alisema nchi wanachama zimekubaliana vipengele vya kufanyia kazi katika rasimu hiyo.
No comments:
Post a Comment