18 January 2012

Yanga kupitisha 'fagio la chuma'

Lengo ni kubana matumizi

Na Amina Athumani

UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umepanga kupunguza matumizi kwa kuwaacha baadhi ya wachezaji na kubakiza 25 pekee, badala ya 30.
Akizungumza Dar es Salam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga, alisema katika kuhakikisha wanapunguza matumizi wataondoa ajira kwa baadhi ya wachezaji, ambao wataonekana hawana msaada na timu hiyo.
Alisema katika mchujo huo hawataangalia mchezaji kujituma tu, bali kuna suala la uwajibikaji na nidhamu pia kwani wanatakiwa kubaki na wachezaji 25 watakaoitumikia timu hiyo vizuri.

Alisema kwa wachezaji waliopelekwa timu nyingine kwa mkopo, wataangalia uwezo wao kama watakuwa wakifanya vyema katika klabu walizopelekwa watarudishwa, lakini kama wakiboronga itakuwa imekula kwao kwani ajira zao zitasitishwa.
Nchunga alisema mwaka huu, wamejipanga kiutekelezaji zaidi na kwamba porojo zote zitakuwa zimefikia kikomo.
Mwenyekiti huyo alisema kwa sasa klabu hiyo, imehakikisha wachezaji wote wamelipwa mishahara yao hadi kufikia Desemba mwaka jana, pamoja na benchi la ufundi na wafanyakazi wa klabu hiyo.
Alisema pia kupitia mikataba walioingia na kampuni mbalimbali, motisha kwa wachezaji itaongezeka zaidi na kuwataka wachezaji wawe watulivu, kwani uongozi wake umekuwa makini katika kutafuta mikataba minono na kwamba suala la kuchelewa kwa mishahara litabaki historia.

No comments:

Post a Comment