18 January 2012

Mkwassa aitolea uvivu serikali

Na Zahoro Mlanzi

KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), Charles Mkwassa ameamua kuivaa serikali na kuitaka isaidie kwa kiasi kikubwa timu hiyo na si kukabidhi bendera na kuondoka.
Mbali na hilo, Mkwassa amesema wanahitaji maandalizi bora tofauti na waliyoyafanya awali kabla hawajaivaa Namibia, vinginevyo hawatasonga mbele kutokana na wapinzani wao kujiandaa vizuri.

Akizungumza Dar es Salaam jana kuhusu safari yao waliyokwenda Namibia, ambako waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya taifa ya wanawake ya nchi hiyo, Mkwassa alisema kama si jitihada binafsi za wachezaji wake wasingepata ushindi huo.

"Namibia ni timu nzuri wala si ya kubeza, imeandaliwa vizuri tofauti na timu yangu, ina wachezaji wanne wanaocheza Ujerumani na ukizingatia walitawaliwa na nchi hiyo basi huduma muhimu zote wanapata," alisema Mkwassa na kuongeza;

"Tatizo walilonalo ni moja tu, hawana ukakamavu na pia waliweka kambi Afrika Kusini, sasa ukiangalia mazingira hayo ni dhahiri walijiandaa vizuri," alisema.

Alisema maandalizi hayo yanatokana na sapoti nzuri ya serikali yao, lakini kwa upande wa Tanzania, sapoti imekuwa ndogo kutoka serikalini zaidi ya kukabidhi bendera na kuondoka.

Kocha huyo alisema ifike wakati sasa serikali ishiriki kwa kiasi kikubwa kuhakikisha timu hiyo, inaandaliwa vizuri zaidi kwani pamoja na maandalizi wanayoyapata, lakini vijana wake wanajituma na kuwatoa kimasomaso Watanzania.

Akizungumzia kuhusu mchezo wa marudiano, Mkwassa alisema kinachotakiwa ni kupewa maandalizi bora, timu hiyo iondokane na suala la kutembeza bakuli kila kukicha na ameishukuru TFF kwa jitihada wanazofanya kuinusuru timu hiyo.

Alisema timu hiyo kwa sasa ndiyo ambayo inalitangaza vizuri taifa katika soka, kwani katika mechi hiyo waliweza kuvunja rekodi kwa kujaza mashabiki wengi kitu ambacho hakijawahi kutokea kwenye Uwanja wa Sam Nujoma nchini humo.

Mabao ya Twiga katika mechi hiyo yalifungwa na Asha Rashid na Mwanahamisi Omari ambapo marudiano itakuwa ni Januria 29, mwaka huu na kambi wanatarajia kuanza leo mjini Mlandizi, Pwani.

No comments:

Post a Comment